0


Serikali yapiga marufuku uingizwaji wa sukari nchini ili kulinda soko la viwanda vya sukari vya ndani
                      
RAIS John Magufuli amesema amedhamiria kwa dhati kufufua viwanda vya ndani na kama mfano amepiga marufuku kwa kiongozi yeyote wa serikali, kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi zaidi yake.
Aidha, amesisitiza kwamba ataendelea kutumbua majipu ya viongozi mafisadi na wala rushwa, kwa kuwa yeye na viongozi wenzake sio wakatili, ila ni kutokana na nchi kuoza.

Amesema yupo radhi kuchukiwa na Watanzania wachache, ambao wamekuwa wakihusika na vitendo vya ufisadi, vinavyoathiri maisha ya Watanzania wengi ili kuiwezesha nchi kusonga mbele kuelekea kwenye uchumi wa kati kwa kasi.
Rais Magufuli alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana, alipokutana na makundi mbalimbali ya wadau walioshiriki kwenye kampeni zake kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na kuibuka na ushindi uliomuwezesha kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Akizungumzia ufufuaji wa viwanda ikiwa ni moja ya eneo alilolitilia msisitizo mkubwa wakati wa kampeni, Rais Magufuli alisema nia yake ya kufufua viwanda ipo pale pale na kusema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.
Akitoa mfano, Rais alisema wakati yapo maeneo ambayo wakulima wanajishughulisha na kilimo cha miwa na zao hilo kuwa tegemeo lao katika kuinua uchumi wao, wapo wafanyabiashara wanaojali maslahi yao binafsi ambao wamekuwa wakiagiza sukari kutoka nje hatua inayosababisha kufa kwa viwanda vya sukari vya ndani.
“Mtu anaagiza sukari kutoka nje, tena wakati mwingine ni sukari ambayo muda wake wa kuisha matumizi umekaribia kumalizika. Huyu mfanyabiashara anaingiza sukari hiyo na kuifungasha upya ili isijulikane kuwa inakaribia kuharibika na kuwauzia wananchi masikini. “Kitendo hiki kinasababisha sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani kukosa soko, wakulima wanakosa soko la miwa yao, na serikali nayo inakosa mapato ya ushuru. Kwa vile bahati nzuri Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) mpo hapa, nasema kuanzia sasa asiwepo mtu wa kutoa kibali cha mtu kuagiza sukari kutoka nje hadi ruhusa hiyo itoke kwangu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mkakati kama huo hautaishia kwenye sukari pekee, bali ni mkakati ambao utahusu maeneo yote ya uzalishaji ili wananchi wa kipato cha chini waneemeke na nchi yao. “Nimekuwa nasema nchi yetu si masikini. Hii nchi ni tajiri sana, lakini wapo watu wamekuwa wanajinufaisha wao. Wapo tayari wapokee virushwa ili waneemeke wao huku Watanzania wengi wakiumia na kuteseka. “Ndio maana nasisitiza kwamba nitaendelea kutumbua majipu ya viongozi mafisadi na wala rushwa.
Tunapotumbua majipu si kwamba sisi ni wakatili hapana, ila ni kutokana na nchi yetu kuoza. Kila unapotupia jicho pameoza, hadi wakati mwingine unashindwa kuamua uanze na jipu lipi na lipi ulitumbue kesho, yapo majipu mengine hayasikii dawa. “Hawa watu wanaolalamika sana sasa ni wachache ambao walikuwa wananufaika na ufisadi na rushwa. Ni bora ukachukiwa na watu 1,000 ili upendwe na watu milioni 50.Kama nitaboresha maisha ya Watanzania milioni 50, hata kwa Mungu tutapokelewa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema serikali yake itaendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya neema na ya uchumi wa kati na kuwa umoja, mshikamano na uzalendo usioambatana na tofauti za kidini, ukabila na itikadi za kisiasa ni nyenzo kubwa katika kufikia mafanikio hayo.
Chanzo cha utumbuaji majipu
Akizungumzia Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi, alipofungua rasmi Bunge mjini Dodoma Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisema “Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
"Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia. Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo."
"Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu."
"Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu."
"Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na mniunge mkono wakati natumbua majipu haya”.

Post a Comment

 
Top