MAJINA ya
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA), waliohusika kutoa makontena 2,431 bila kulipa ushuru
kati ya Machi hadi Septemba 2014 katika Bandari ya Dar es Salaam,
yamepatikana na kufikishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Taarifa
zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa wahusika wote walioshiriki
katika hujuma hiyo, majina yao yameshafikishwa kwa Waziri Mkuu na
kinachoendelea ni uchunguzi wa kila mmoja wao.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufanya ziara ya ghafla
wiki hii katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo alisema makontena hayo
2,431, yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu (ICD) nne ambazo
ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kutokana
na taarifa hiyo, Waziri Mkuu alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel
Mhanga, ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi
huo, ambapo jana ilithibitishwa kuwa kazi hiyo imekamilika na
kinachofanyika ni uchunguzi wa watuhumiwa.
Mbali na
kupeleka majina hayo, Mhanga pia alipewa wiki moja inayoisha Alhamisi ya
wiki ijayo, kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji
malipo wa sasa bandarini na kuweka mfumo mpya wa malipo wa
kielektroniki (e-payment). Uchunguzi Ingawa haijajulikana aina ya
uchunguzi unaofanyika dhidi yao, lakini ni wazi moja ya hatua hizo za
kiuchunguzi, itahusu namna walivyohusika na ukaguzi wa mali zao.
Tayari
uchunguzi wa aina hiyo, umeshaanza kufanyika kwa watuhumiwa wa utoaji wa
makontena 329 yaliyokuwa kwenye ICD ya Azam, ambayo yanakadiriwa
kuipotezea Serikali zaidi ya Sh bilioni 80, ambapo taarifa zimeonesha
kuwa baadhi walikaguliwa mpaka katika majumba yao.
Waziri
Mkuu Majaliwa alipokwenda bandarini kwa mara ya kwanza kupitia ziara ya
kushtukiza na kuibua upotevu wa mapato katika makontena hayo 329,
aliagiza mali za watuhumiwa hao zichunguzwe, kama zinalingana na mapato
ya mtumishi wa umma.
Aidha
wiki hii katika utekelezaji wa agizo hilo, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA,
Dk Philip Mpango, aliagiza watumishi wote wa mamlaka hiyo, kuwasilisha
taarifa sahihi ya orodha ya mali zote wanazomiliki kwa ajili ya uhakiki
wa kina. Watumishi hao wametakiwa kuwasilisha taarifa hizo kwa uongozi
wa juu wa mamlaka hiyo ifikapo Desemba 15 mwaka huu.
Agizo
hilo limeambatana na onyo kuwa mtumishi yeyote, atakayebainika kuhusika
na vitendo vyovyote vya ubadhirifu, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu
kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi, kulingana na makosa
atakayokutwa nayo.
Wengi
kupoteza kazi Hatua hiyo inazidisha wasiwasi wa kuongezeka watumishi wa
Serikali walio katika hatari ya kusimamishwa kazi, baada ya wenzao 36
kusimamishwa kazi wiki hii na wiki iliyopita.
Walioanza
kusimamishwa kazi Ijumaa ya wiki iliyopita walikuwa Kamishna wa
Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu
Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama), Haruni Mpande; Hamisi Ali Omari (hakutajwa ni wa idara gani)
na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
Siku hiyo
hiyo waliyosimamishwa kazi vigogo hao, Rais John Magufuli,
akamsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kesho yake
wakaongezwa watumishi wengine watatu; ambao ni Anangisye Mtafya,
Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Kabla
hali haijatulia, Alhamisi ya wiki hii watumishi wengine 27 wa TRA,
walikamatwa katika geti namba tano na kusimamishwa kazi, kisha wakawekwa
rumande kupisha uchunguzi wao.
Kortini
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, juzi maofisa waliosimamishwa kazi
Ijumaa ya wiki iliyopita kwa upotevu wa mapato katika makontena hayo
329, akiwemo Masamaki (56), Mponezya (45), Mpande (28), Omari (48) na
Eliachi (31), walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh
bilioni 12.7.
Washtakiwa
hao pamoja na wafanyakazi wengine wa ICD ya Azam, walifikishwa
mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Huruma Shahidi. Mbali na hao watumishi wa TRA, wengine waliopanda
kizimbani kwa makosa hayo ni wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam,
akiwemo Mkuu wa Ulinzi na Usalama, Raymond Louis (39) na Meneja Ashraf
Khan (59).

Post a Comment