Mwaandishi wetu LIWALE
WANANCHI wilayani Liwale mkoani Lindi wameshauriwa kuanza utamaduni wa kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Gaudes Nyamiula wakati alipokuwa anafungua semina ya wataalam kuhusu uratibu wa utekelezaji miradi ya ajira ya muda chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini Tasaf awamu ya tatu katika ukumbi wa kituo cha walimu wilayani humo.
Nyamiula alisema sehemu kubwa ya wilaya Liwale inapata mvua za wastani na sehemu nyingine mvua za kutosha lakini hata hivyo wananchi wameshidwa kutumia maji ya mvua kwa faida ikiwemo kwenye miradi ya uzalishaji , kilimo na mifugo.
Aidha mkurugenzi huyo amewataka washiriki kuwa wavumilivu na kuacha tabia ya kuvaa kofia kutoa maamuzi bali wakaziwezeshe jamii kutambua vipaumbele vinavyogusa maisha yao ya kila siku na vizazi vijavyo.
Kwa upande Afisa maendeleo ya jamii kutoka Tasaf makao makuu Amos Mkude alisema lengo kubwa la warsha hiyo ni kutoa mafunzo ya timu ya wawezeshaji kwenye maeneo ya utekelezaji kuhusu miradi ya kutoa ajira ya muda ili waweze kuwaelimisha jamii hatua zitakazo takiwa kufuatwa ili walengwa wapate ajira ya muda na kuongeza mapato.
Wanafanyakazi wa vitengo mbalimbali wa Halmashauri wilaya wakiwa kwenye semina ya wataalam kuhusu uratibu wa utekelezaji miradi ya ajira ya muda chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini Tasaf awamu ya tatu katika ukumbi wa kituo cha walimu wilayani humo.
Post a Comment