0

Dar es Salaam. Leo ni kufa
au kupona kwa makada wa
CCM wanaowania ubunge
wakati wanachama wa
chama hicho tawala
watakapopiga kura
wilayani kuchagua
wagombea kwenye majimbo
yao baada ya wiki kadhaa
za vikumbo zilizojumuisha
kurushiana ngumi, tuhuma
za rushwa, malumbano na
migomo.
Uchaguzi Mkuu umepangwa
kufanyika Oktoba 25
mwaka huu.
Katika upigaji kura leo,
wanachama watakuwa na
kazi ngumu kuamua kuhusu
makada waliogeukia
ubunge baada ya kukosa
urais, mawaziri katika
Serikali ya Awamu ya Nne
inayoondoka madarakani,
waliotemwa mwaka 2010
wanaowania kurejea
bungeni, wakuu wa wilaya
ambao wameingia kwa
wingi kwenye mbio hizo, na
pia wabunge wanaomaliza
muda wao ambao ama
walikidhi mahitaji yao au
kutofanya kazi ipasavyo.
Mchakato huo wa kura ya
maoni unafanyika baada ya
kumalizika kwa siku 10 za
wagombea hao kujinadi
kwa makada wenzao katika
kata mbalimbali za
majimbo wanayotaka
kugombea, huku baadhi
wakijitoa kutokana na
kushindwa kulipa fedha
kama mchango wao wa
safari za kampeni.
Mchakato wa kura za
maoni, utafuatiwa na vikao
vya kamati za siasa za
wilaya na mikoa wakati
kikao cha Halmashauri Kuu
ya CCM kitafanyika kwa
siku mbili kuanzia Agosti 11
kwa ajili ya uteuzi wa
wagombea rasmi wa
ubunge na udiwani wa
CCM.
Gazeti hili linakuchambulia
maeneo matano
yatakayozua mjadala mkali
mara baada ya matokeo ya
kura ya maoni kutangazwa,
pamoja na kilichojitokea
wakati wa kampeni za
wagombea hao.
Wagombea urais
waliojitosa ubunge
Macho ya wana-CCM na
wananchi wengine
yatakuwa yakielekezwa
kwa makada wa CCM
walioanguka kwenye mbio
za urais na ambao
wamegeukia ubunge, ambao
ni pamoja na Mwigulu
Nchemba (Iramba
Magharibi), Lazaro
Nyalandu (Singida
Kaskazini) na mwanasiasa
mkongwe ambaye kwa sasa
ni Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven
Wasira.
Wengine ni aliyekuwa
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ambaye alijiuzulu
kutokana na kashfa ya
escrow, lakini anataka
kurejea bungeni
kuwakilisha jimbo la
Musoma Vijijini.
Pia yumo January Makamba
wa Bumbuli mkoani Tanga,
William Ngeleja
(Sengerema), Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe
(Nachingwea), Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Dk Titus Kamani
(Busega) na Waziri wa
Afrika Mashariki, Dk
Harrison Mwakyembe
anayerudi Kyela mkoani
Mbeya na Balozi Augustine
Maiga anayewania Iringa
Mjini.
Majimbo yenye mchuano
mkali
Nzega Vijijini
Moja kati ya majimbo yenye
upinzani mkali kwa sasa ni
jimbo la Nzega Vijijini
kutokana na uwepo wa
makada wawili wa chama
hicho, Lucas Selelii na Dk
Hamisi Kigwangalla.
Katika uchaguzi uliopita wa
2010, makada hao
walivaana lakini wote
wakaangushwa na Hussein
Bashe aliyeibuka wa
kwanza akifuatiwa na
Selelii, lakini Halmashauri
Kuu ya CCM ikamchukua Dk
Kigwangalla aliyekuwa
mshindi wa tatu.
Mgawanyo wa majimbo
uliofanywa hivi karibuni na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), umefanya
mpambano huo uwe wa
makada hao, baada ya
kumwachia Bashe jimbo la
Nzega Mjini.
Iringa Mjini
Jimbo jingine lenye
mchuano mkali ni Iringa
Mjini ambako Balozi
Augustine Mahiga
aliyekwama katika harakati
za kuwania urais kupitia
CCM, atapambana na
makada wengine kuwania
kupata tiketi ya kulikomboa
jimbo hilo kutoka Chadema.
Makada wengine kati ya 12
wanaowania kiti hicho ni
Mkuu wa Wilaya ya
Wanging’ombe, Frederick
Mwakalebela, mwenyekiti
wa CCM wa mkoa, Jesca
Msambatavangu na katibu
mwenezi wa CCM mkoa wa
Iringa, Dk Yahya Msigwa.
Kundi lingine ambalo
huenda likaleta upinzani
katika uchaguzi huo
linamjumuisha mjumbe wa
NEC wa Iringa Mjini,
Mahamoud Madenge,
mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe, Falles Kibassa
na mwandishi wa habari,
Frank Kibiki.
Wengine wanaowania
Iringa Mjini ni Peter
Mwanilwa, Frank Kibiki,
Michael Mlowe, Nuru
Hepautwa, Adestino
Mwilinge na Adani Kiponda.
Jimbo la Mkalama
Jimbo la Mkalama
linaongoza kwa kuombwa
na makada 16 wakiongozwa
na mwenyekiti wa mkoa wa
Singida, Mgana Msindai,
Profesa Shaaban Aman
Mbogho, Nakey Samwel
Sule, Orgenes Emmanuel,
Joseph Mbasha na Allan
Joseph Kiula.
Wengine wanaowania jimbo
hilo ni Emmanuel Mkumbo,
Dk Kissui Stephen Kissui,
William Makali, Kyuza
Kitundu, Dk Charles Mgana,
Salome Mwambu, Francis
Mtinga, Dk George Mkoma
na Lameck Itungi.
Jimbo la Kalenga
Mchuano mkali pia upo,
Kalenga linalowaniwa na
mbunge wa sasa, Godfrey
Mgimwa na Jackson
Kiswaga, na Mkuu wa Mkoa
wa Mbeya, Abbas Kandoro
na mbunge wa zamani wa
jimbo hilo, George Mlawa.
Jimbo la Mwanga
Mshikemshike mwingine
unatarajiwa kuibuka katika
Jimbo la Mwanga ambako
Waziri wa Maji, Profesa
Jumanne Maghembe
anapambana tena na
hasimu wake mkubwa
katika kiti hicho, Joseph
Thadayo.
Maeneo yaliyotokea
tafrani
Wakati baadhi
wakikabiliana na upinzani
mkali, makada wengine
watakuwa wakihangaika
kushawishi wapigakura
baada ya kukumbana na
hali ngumu kwenye
kampeni.
Baadhi yao ni mbunge wa
Muleba Kusini, Profesa
Anna Tibaijuka, Harrison
Mwakyembe (Kyela) na
Assumpter Mshama
(Nkenge).
Profesa Tibaijuka
Profesa Tibaijuka
anayewania jimbo hilo kwa
mara ya pili, alishushwa
jukwaani kwa kuzomewa na
wananchi wake katika kata
ya Nshamba wilayani
Muleba na tafrani hiyo
kudumu kwa dakika
kadhaa na kusababisha
wagombea wengine
kulazimika kuondoka.
Kwa mara ya kwanza
alizomewa Juni 8, wakati
wa ziara ya katibu mkuu
wa CCM, Abdulrahman
Kinana kwenye kata hiyo
hiyo kutokana na kutajwa
kwenye kashfa ya escrow
na kushindwa kutekeleza
ahadi ya kuwajengea
barabara ya lami.
Mwakyembe
Hasira za wananchi pia
zilimkumba mbunge wa
Kyela, Harrison
Mwakyembe kwenye moja
ya mikutano yake baada ya
wananchi kupiga kelele
kutotaka kumsikiliza.
Profesa Maghembe
Hali kama hiyo ilimkuta
Profesa Maghembe kwenye
jimbo lake la Mwanga
wakati akijinadi katika
mkutano wa kampeni
uliofanyika Kisangara.
“Kidumu Chama cha
Mapinduzi. Kisangara
saafii,” alisalimia Profesa
Maghembe na kuitikiwa na
sauti za “ondoka ondoka,
tumekuchoka sasa, nenda
kapumzike huna jipya,
waachie wenzio”.
Profesa Maghembe
alipoulizwa na gazeti hili
jana kuhusu kadhia hiyo,
alisema vijana
waliomzomea walikodishwa
na kupewa pombe katika
baa ya jirani ili tu kujaribu
kuchafua hali ya hewa.
Profesa Maghembe
anachuana tena na
mshindani wake wa 2010,
Joseph Tadayo na
wagombea wengine ambao
ni Karia Magaro, Baraka
Lolila, Ramadhani Mahuna,
Japhar Mghamba na Miniel
Kidali.
Naibu Spika Ndugai
Wakati Maghembe
akikumbana na hasira za
wananchi, Naibu Spika wa
Bunge Job Ndugai
alishindwa kuzuia hasira
zake wakati maneno ya
mgombea mwenzake
yaliposababisha amvamie
na kujikuta akihojiwa na
polisi.
Ndugai alihojiwa na polisi
kwa tuhuma za
kumshambulia mgombea
mwenzake, Dk Joseph
Chilongani kwenye mkutano
wa kampeni akimtuhumu
kurekodi tukio la kutaka
kumpiga mgombea
mwingine aliyekuwa
akijieleza na kuponda
uongozi unaomaliza muda
wake.
Hata kama atapita leo,
suala lake linatarajiwa
kuwa moja ya hoja kwenye
kikao cha Halmashauri Kuu.
Mwigulu Nchemba
Hali kama hiyo ipo kwa
mbunge wa Iramba
Magharibi, Mwigulu
Nchemba anayetetea jimbo
lake akipambana vikali na
katibu mkuu wa zamani wa
Wizara ya Nishati na
Madini, David Jairo, pamoja
na Juma Hassan Kilimba
anayerudi na Amon Gyuda.
Nchemba amekumbana na
tafrani baada ya kuhojiwa
na Takukuru kwa tuhuma
za rushwa. Baadhi ya
wagombea wanaowania
pamoja naye walishtaki
kuwa mwenzao anafanya
vitendo ambavyo
walivihusisha na rushwa na
hivyo Takukuru kuchukua
hatua.
Lusinde ‘Kibajaji’
Ushindani mkubwa katika
jimbo la Mtera unaonekana
kuwa baina ya mbunge
anayemaliza muda wake,
Livingstone Lusinde
‘Kibajaji’ na mtoto wa
aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Samuel
Malecela.
Lusinde pia amekuwa
akikumbana na kadhia hiyo
baada ya wananchi
kumzomea wakati akieleza
sera zake kwenye kijiji cha
Nkwenda wilayani
Chamwino.
Baada ya zomeazomea hiyo,
mbunge huyo anadaiwa
kuagiza kikundi cha vijana
kuwashambulia wananchi
ambao walikuwa
wakimpiga kelele
kumzomea.
Venance Mwamoto
Kada mwingine anayewania
kurejea bungeni ni
mwanasoka wa zamani,
Venance Mwamoto ambaye
amerejea Jimbo la Kilolo
kupambana na mbunge wa
sasa Profesa Peter Msolla.
Wanahabari wapambana
Wakati wanahabari
wakikumbana na makada
wa fani nyingine kwenye
mbio hizo, Jimbo la Chemba
linakutanisha wanahabari
wawili, Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Juma Nkamia
ambaye atavaana na
mhariri kutoka gazeti la
Mtanzania, Khamis Nkyota
anayelitaka jimbo hilo kwa
udi na uvumba.
Tayari Nkamia
ameshalalamikia bungeni
harakati za mwanahabari
mwenzake kwenye jimbo
hilo.
Manyoni Magharibi
Hali ushindani inayotokana
na makada wengi
kujitokeza pia ipo kwenye
Jimbo la Manyoni
Magharibi ambako John
Lwanji, mbunge
anayemaliza muda wake,
anakabwa koo na binamu
yake Eliphas Emmanuel
Lwanji. Wengine ni Jamal
Kuwingwa, Jane Likuda,
Mohamed Makwaya,
Yahaya Masare, Athumani
Masasi, Yohana Msita,
Moshi Mmanywa, Adimini
Msokwa, Dk Mwanga
Mkayagwa, Rashidi Saidi na
Francis Shaaban.
Mbeya Mjini
Hali kama hiyo pia ipo
Mbeya Mjini ambako
Charles Mwakipesile
aliyepambana na mbunge
wa sasa Joseph Mbilinyi
mwaka 2010, atakuwa
akipambana na Stephen
Mwakwenda, Nwaka
Mwakisu, Aggrey
Mwasanguti na Mchungaji
Jackson Numbi
Wengine ni Ibrahim
Mbembela, Fatma Ismail ,
Shambwe Shitambala,
Solomon Swila, James
Mwampondele, Ulimboka
Mwakilili, Samuel
Mwaisume, Eliud
Mwaiteleke, Michael Mbuza
Aman Kajuna na Shadrack
Mwakombe.
Singida Kaskazini
Lazaro Nyalandu atakuwa
na kazi ya kuzuia kazi ya
Amos Makiya, Justin Monko,
Michael Mpombo, Sabasaba
Manase, Yahana Sinton,
Mugwe na Aaron Mgogho.
Jimbo la Nanyumbu
Mgombea wa jimbo la
Nanyumbu Dastani Mkapa
yupo katika wakati mgumu
kutokana na mgombea
mpinzani wake William Dua
kuonekana ana kasi ya
kuchukua Jimbo hilo.
Jimbo la Ndanda
Mgombea wa jimbo jipya la
Ndanda, Mariam Kasembe
alijikuta akitoa machozi
baada ya wananchi wa
jumbo hilo kuuliza maswali
kwa mgombea huyo na
kushindwa kuyatolea
majibu.
Jimbo la Newala
Mbunge wa jimbo hilo,
George Mkuchika ana
wakati mgumu kurudi
katika nafasi hiyo kutokana
na ushindani uliopo kuwa
mkubwa ukilinganisha na
uchanguzi wa 2010.
Imeandikwa na Fidelis Butahe,
Mary Sanyiwa, Lauden
Mwambona, Sharon Sauwa,
Gasper Andrew na Geofrey
Nyang’oro.MWANANCHI

Post a Comment

Emoticon
:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top