Mkurugenzi wa Uchaguzi,Kailima Ramadhan
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uhakiki wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mkoa wa Dar es Salaam utaanza Agosti 18 mwaka huu.
Awali zoezi hilo lilitarajiwa kufanyika mkoani humo kuanzia Agosti 15 hadi 19 lakini ilishindikana kutokana na changamoto ya mifumo ya kompyuta iliyojitokeza.
Taarifa iliyotolewa jana na tume hiyo na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan ilieleza kuwa zoezi hilo litaanza rasmi kwa daftari hilo kutolewa wazi kwa waliojiandikisha kuanzia Agosti 18 hadi 22 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam waliojiandikisha wanapaswa wajitokeze kwa wingi kuanzia Agosti 18 kuhakiki taarifa zao.
Ilieleza taarifa hiyo kuwa, kujitokeza mapema na kwa wakati kutasaidia kubaini kama kuna mapungufu yoyote ili yafanyiwe kazi kabla ya kuchapisha daftari hilo kwa ajili ya kutumika kwenye uchaguzi mkuu. Daftari hilo linatarajiwa kutolewa wazi kwa waliojiandikisha katika ofisi zote za Kata au Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.
Wananchi pia wametakiwa kutumia simu za mkononi kwa kupiga *152*00# kisha wafuate maelekezo ili kuhakiki taarifa zao.
Baadhi ya wananchi waliojiandikisha walionekana katika vituo vya kujiandikisha kuhakiki majina yao wakitumia taarifa za awali zilizoeleza kuwa uhakiki ulikuwa ufanyike Agosti 15 hadi 19 mwaka huu.
Hata hivyo vituo vingi na watendaji wengi wa Kata waliwajibu baadhi ya wananchi kuwa hawana taarifa na hatua ya uhakiki kuanza katika mkoa wa Dar es Salaam.
Post a Comment