Bunge la 10 likielekea ukingoni baada ya
kupitisha Bajeti ya Serikali leo, mambo
matatu mazito
Dar/Dodoma . Bunge la 10 likielekea
ukingoni baada ya kupitisha Bajeti ya
Serikali leo, mambo matatu mazito
yametajwa kama ‘madudu’ yaliyoleta
mtikisiko na kuonekana kama ishara ya
kuisimamia Serikali na kusababisha baadhi
ya mawaziri kupoteza nafasi zao.
Mambo hayo ni matokeo ya ripoti za
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali
(CAG), Operesheni Tokomeza na ufisadi
katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, pamoja na kutaja kashfa hizo,
baadhi ya wabunge waliozungumza na
Mwananchi wamelichambua Bunge hilo
kwa mitazamo tofauti baadhi wakimsifia
Spika Anne Makinda kuwa alisimamia
kanuni na wengine wakimkosoa kwa
kuilinda Serikali.
Bunge hilo lililozinduliwa Novemba 18,
2010 kwa Rais Jakaya Kikwete kulihutubia,
anatarajia kulihutubia tena kwa hotuba ya
mwisho, kati ya Julai 9 na 10, mwaka huu
na kulivunja kwa kwa mujibu wa sheria
kupitia Tangazo la Serikali (GN).
Ripoti ya CAG
Mwaka 2012, Bunge hilo likiwa na miaka
miwili tu, CAG alitoa ripoti iliyoonyesha
ufisadi mkubwa Serikalini na mawaziri
kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia
mali za umma.
Ripoti hiyo ilizua mjadala mzito bungeni
na wabunge wakashinikiza baadhi ya
mawaziri wajiuzulu kutokana na
kushindwa kuwajibika.
Baada ya mvutano mkali Rais Kikwete
alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
baada ya kuwatema mawaziri sita na naibu
mawaziri wawili.
Operesheni Tokomeza
Sakata jingine lililoteka Bunge hilo ni ripoti
ya Operesheni Tokomeza Ujangili
iliyoanzishwa na serikali kwa lengo la
kukomesha ujangili nchini.
Operesheni hiyo ililalamikiwa na wabunge
kuwa utekelezaji wake ulivunja sheria,
kanuni na taratibu.
Bunge kupitia kamati ndogo iliyotokana na
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira ilichunguza
operesheni hiyo na kubaini uvunjifu
mkubwa wa sheria.
Katika sakata hilo mawaziri wanne
walitimuliwa na Januari 19, 2014 Rais
Kikwete akateua wawili wapya na naibu
mawaziri wanane, huku akiwapandisha
vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa
mawaziri kamili.
2. Akaunti ya Escrow
Sakata la uchotwaji wa fedha katika
Akaunti ya Tegeta Escrow liliibuliwa na
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-
Mageuzi), David Kafulila baada ya kufichua
ufisadi uliohusisha uchotwaji wa Sh306
bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili
walipoteza nyadhifa zao pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali kuwahusisha na sakata hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali
walisimamishwa au kufunguliwa mashtaka
kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi
huo.
Kauli za wabunge
Mbali na matukio hayo, baadhi ya wabunge
wamesema katika Bunge hilo walijitahidi
kuwa wamoja katika masuala yanayoligusa
Taifa, ingawa wakati mwingine
walitofautiana kwa sababu kadhaa
zikiwamo za kiitikadi.
Moja ya mambo waliyoainisha kama kasoro
za Bunge hilo ni usimamiaji usioridhisha
wa Serikali katika utekelezaji wa bajeti
unaosababisha fedha zinazotengwa kutofika
kwa wakati, kutofika kabisa au kufika
pungufu katika maeneo zilikopangwa.
Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman
Khalifa (CUF), alisema pamoja na
kumpongeza Spika Anne Makinda kwa
kutekeleza mambo mengi
yaliyopendekezwa, kuna baadhi ya mambo
ambayo yameachwa bila ya kujua iwapo ni
kwa makusudi au kwa bahati mbaya.
Alipoulizwa ni mambo gani alisema baadhi
ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata la
Escrow hayajafika mwisho.
Mbunge wa Makunduchi (CCM), Samia
Suluhu Hassan alisema Bunge la 10
lilikuwa na changamoto za vijana ambao
walikuwa wakiwachemsha, lakini pamoja
na yote walishindana ndani ya ukumbi,
lakini nje ya bunge wote walikuwa
wamoja.
Alisema mafanikio ya Bunge hilo, wabunge
watakaokuja katika Bunge la 11
wanatakiwa kuyaendeleza.
Alimsifu Spika Makinda kwa kazi nzuri na
kumwelezea kuwa hakuwa akibabaika
inapotokea presha za wapinzani hata
ilipotokea wanasusia vikao.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi
Magharibi, David Silinde (Chadema)
alisema Bunge la 10 linamaliza muda wake
likiwa limeweka heshima kubwa kwa
Watanzania kwa kushughulikia kashfa
kubwa za ufisadi.
Silinde alitolea mfano wa masuala ya
Escrow, Operesheni Tokomeza na mengine
ambayo yaliibuliwa katika bunge hilo
alilosema lilikuwa limesheheni vijana
waliokuwa na mchango mkubwa katika
kuibua mambo ya msingi.
Hata hivyo, alisema kuwa hawakufikia
mwisho kutokana na maazimio mengi ya
Bunge kuachwa bila ya kutekelezwa kama
ilivyokusudiwa.
Akizungumzia spika ajaye, Silinde
alipendekeza awe walau na taaluma ya
sheria ili aweze kujua mambo ya kanuni na
sheria kwa upana wake.
Mbunge mwingine kijana, Moses Machali
(Kasulu- NCCR-Mageuzi) alisema Bunge la
10 halikuwa la msisimko kwa kuwa Spika
Makinda alikuwa akiibeba zaidi Serikali na
CCM na chombo hicho kushindwa kuibana
Serikali pale ilipokosea.
Alisema Spika wa Bunge la Tisa, Samuel
Sitta alikuwa akitoa nafasi sawa
ukilinganisha na Makinda, hali aliyosema
ilisababisha Bunge kuyumba.
Kwa upande wake, Prudencia Kikwembe
(Viti Maalumu – CCM) alisema Bunge hilo
lilifanya kazi kwa nafasi yake lakini
likakabiliwa na changamoto ya ushabiki
wa vyama badala ya maslahi ya Taifa.
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum
Barwani yeye analia na mfumo wa kikatiba
ambao anasema kuwa ulisababisha Bunge
kuwa sehemu ya Serikali.
Barwani pia alieleza kuwa hata Spika wa
sasa alishindwa kutimiza majukumu yake
ipasavyo kutokana na mfumo wa kikatiba
uliopo.
Akitoa maoni yake kuhusu Spika ajaye,
alisema awe ni kiongozi mwenye busara
lakini atambue kuwa chombo hicho ni
mhimili unaojitegemea.
Hezekia Chibulunje, (Chilonwa – CCM)
alisema Bunge la 10 lilikuwa la
ushirikishwaji kwa kuwa uchangiaji
ulikuwa mkubwa na Spika alitoa nafasi
kwa kila upande bila upendeleo.
Alisema baadhi ya wabunge walikuwa
makini kuwasilisha ujumbe kwa kuwa
walikuwa wakionekana moja kwa moja
kupitia runinga.
Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Ibrahim
Saanya alisema Bunge limefanya kazi yake
lakini tatizo linakuja katika utekelezaji wa
bajeti.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
Kigoma (NCCR-Mageuzi) alisema sehemu
kubwa ya Bunge la 10 lilitawaliwa na
vijana na wameweza hiyo kazi.
Alisema kuwa uchache wa wapinzani
umewafanya wawe wanyonge katika
kufikia uamuzi wa jumla.
Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini, CCM),
alisema Bunge hilo lilikuwa la mafanikio
kwa kuwa mengi yalitimizwa na kwa kuwa
walikuwa wanaonekana kupitia TV,
walifanya hadaa ili kuwaaminisha
wananchi masuala ambayo baadhi ni ya
uongo na hayawezekani.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim
Bakari na Habel Chidawali.Chanzo:Mwananchi
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.