0
WANAWAKE wa kijiji cha Ibihwa Wilaya
ya Bahi mkoani Dodoma wameomba
kuongezewa vitanda vya kujifungulia
kutokana na zahanati wanayotumia kuwa
na kitanda kimoja na kulazimika kupanga
foleni ili wapate nafasi pindi
wanapopatwa na uchungu.
Kilio cha wanawake hao kilitolewa mbele
ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis
Mwonga alipokuwa akipokea kero kutoka
kwa wananchi wa kijiji hicho zilizotolewa
na Ofisa Mtendaji wa kata ya hiyo ya
Ibihwa, Jenifer Masaulwa kwenye
mkutano wa hadhara.
Masaulwa alisema zahanati hiyo ina
kitanda kimoja hali inayolazimu
wajawazito kupanga foleni kusubiri, hali
ambayo inafanya wakati mwingine
wanawake wengine kujifungulia chini
wanapopatwa na uchungu wakati kitanda
hicho kikitumiwa na mzazi mwingine.
“Huduma kwa wanawake wanaojifungua
siyo nzuri kutokana na wajawazito
kusubiriana na wakati mwingine ikiwa
umechelewa itakulazimu kujifungulia
kwenye godoro linalolaliwa kwa ajili ya
kupumzikia,” alisema.
Aliitaja changamoto nyingine
inayowakabili ni kukosekana kwa sehemu
ya kuhifadhia takataka za akina mama
wanaojifungulia hali inayohatarisha afya
ya wanawake na watoto wanaozaliwa na
jamii kwa ujumla.
Mmoja wa wanawake wa kijiji hicho, Mary
Gasper alisema ni muhimu jambo hilo
likapewa uzito wa pekee ili waweze
kuongezewa vitanda ili wajifungue katika
mazingira salama zaidi.
Akizungumza na wananchi hao Mkuu
huyo wa wilaya, aliwataka wananchi wa
kata hiyo kushirikiana na halmashauri ili
waweze kujenga chumba kwenye eneo
lililopo la zahanati.
Alisema kwa kushirikiana huko wanaweza
kutatua kero hiyo utawawezesha
kukamilisha haraka kupata kliniki
itakayoondoa tatizo la uhaba wa eneo la
kujifungulia wanawake wajawazito.

Post a Comment

 
Top