0

Uongozi wa Yanga umetangaza rasmi kumtema kipa Juma Kaseja huku ukijipanga kumshtaki ili aulipe Sh. milioni 340 kutokana na kuvunjika kwa mkataba huo.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana mchana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema klabu hiyo imeamua kuachana na kipa huyo chaguo la kwanza la zamani la Taifa Stars kutokana na kukiukwa kwa masharti ya mkataba.
“Kutokana na hali iliyotokea Yanga imeamua kumwacha kipa Juma Kaseja. Kama yeye alimwaga mboga, na sisi (Yanga) tunamwaga ugali,” alisema Muro.
Muro alisema kuwa Novemba 8, 2013, usajili miaka miwili wa Kaseja Yanga ulifanyika akipewa Sh. milioni 20 za utangulizi kati ya Sh. milioni 40 za ada ya kusaini mkataba kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Aliendelea kufafanua kuwa Januari Mosi, 2014 Yanga ilimlipa Kaseja Sh. milioni 20 alizokuwa akiidai kama ada ya usajili.
Hata hivyo, Muro alisema kuwa Kaseja aliwasilisha barua Yanga Novemba 11, 2014 akilalamika kutopangwa mara nyingi kwenye kikosi hicho cha wanajangwani huku pia akitaka kukatiwa bima.
“Desemba 12, 2014 Yanga ilimjibu Kaseja kwamba taratibu zote anazijua kuhusu masuala ya bima za matatizo makubwa ya wachezaji (serious injuries) na kumkumbusha kuwa suala kupangwa kikosini liko chini ya benchi la ufundi.
“Isitoshe Kaseja alipangwa katika mechi nyingi za Yanga, alicheza dhidi ya Mtibwa Sugar, CDA ya Dodoma na timu moja ya Shinyanga. Katika michezo tunajua mchezaji hawezi kuwa ‘fiti’ wakati wote.
“Desemba 31, 2014 akaleta barua nyingine akidai suala la bima na kutopangwa katika mechi nyingi. Tukaona Juma Kaseja hana hoja za msingi, kama imeshalipwa, kwa nini aendelee kuwa hivyo? Tukaona hapa kuna kitu.
“Sasa, msimamo wa klabu tunamwacha aende zake. Usipoonekana katika kambi na mazoezi ya timu yetu kwa siku mbili bila kutoa taarifa, kwa mujibu wa mikataba ya Yanga na wachezaji, unakuwa umevunja mkataba,” alisema zaidi Muro aliyekuwa amefuatana na kocha mkuu Mholanzi Hans van der Pluijm na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Taarifa zaidi  kutoka ndani ya uongozi wa Yanga jana mchana, zilieleza kuwa kutokana na kuvunjika kwa mkataba huo, Yanga inafungua mashtaka dhidi ya Kaseja ikimtaka arudishe Sh. milioni 40 za ada ya usajili na Sh. milioni 300 kama fidia baada ya kusababisha kuvunjika kwake.
Kaseja tayari amesema kupitia mawakili wake kwamba Yanga ndiyo waliokiuka mkataba kwa kumlipa kimyakimya kwa kumuingizia katika akaunti yake bila ya kumtaarifu kinyume cha maafikiano Sh. milioni 20 za mwisho za ada yake ya usajili ikiwa miezi mingi tayari imepita tofauti na muda wa makubaliano yao.
 NIPASHE

Post a Comment

 
Top