TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ufafanuzi kuhusu Tume ya Katiba kutupiwa virago
Ufafanuzi kuhusu Tume ya Katiba kutupiwa virago
Gazeti la Raia Mwema lililotoka
leo, Jumanne, Aprili 2, 2014, limeandika habari zisizokuwa za kweli
chini ya kichwa cha habari : “Warioba: Ikulu imetutupia virago”.
Habari hiyo inamkariri aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba akidai kuwa Tume yake ilifukuzwa kazi, kwamba haikupewa muda wa
kuandaa na kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba
wajumbe wa Tume hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Aidha, Gazeti la Mtanzania la leo pia, limeandika habari, zisizokuwa za kweli vile vile, chini ya kichwa cha habari: “Bilioni 6 kuipoza Tume ya Warioba”.
Habari hiyo inamkariri mjumbe
mmoja wa Tume hiyo, ambaye Gazeti halimtaji jina, akidai kuwa Tume hiyo
inatarajiwa kupewa kiasi cha Sh.bilioni sita ikiwa ni kiinua mgongo
ambako kila mjumbe atapata kiasi cha Sh. milioni mia mbili.
(a) Tume kufukuzwa kazi
Itakumbukwa kuwa moja ya mijadala
mikali ya awali kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya ulihusu lini Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake; wengine wakitaka Tume imalize
muda wake baada ya kukabidhi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba,
wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya Mwenyekiti wake Jaji
Warioba kuwasilisha Rasimu yake Bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe
wa Tume wawe sehemu ya Bunge Maalum la Katiba.
Hatimaye, ilikubaliwa kuwa
Shughuli za Tume zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti wake
kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba kama
inavyoelekezwa katika Kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Kifungu hicho kinasema kuwa baada
ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum chini ya
Kifungu cha 20(3) (cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba) Rais, kwa Amri
itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, atavunja Tume.
Mheshimiwa Warioba aliwasilisha
Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba Jumanne ya Machi 18,
mwaka huu, 2014 na siku iliyofuata Jumatano, Machi 19, 2014 na kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alitia saini tangazo la
Serikali la Kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tangazo hilo
lilichapishwa katika toleo lililofuata la Gazeti la Serikali la Ijumaa,
Machi 21, 2014. Gazeti la Serikali huchapishwa kila Ijumaa ya kila wiki.
Hivyo, tokea mwanzo wa mchakato
mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
hapakupata kuwepo, hata wakati mmoja, shaka kuhusu siku ya Tume hiyo
kumaliza kazi zake. Mwenyekiti wa Tume, wajumbe wote wa Tume,
Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua fika siku ya mwisho ya
Tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo leo
ni kiwango cha juu sana cha unafiki.
Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka
wala mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo. Hivyo, madai ya Ikulu
kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni
jambo la kutunga tu.
(b) Muda wa kuandaa na kukabidhi nyaraka na ofisi
Hili nalo ni jambo la kutunga na
kuzusha tu. Mheshimiwa Jaji Warioba alikabidhi rasmi Ripoti ya Tume na
Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein, Jumatatu ya Desemba 30, 2014, mbele ya wananchi viwanja vya
Ukumbi wa Karimjee, Dar Es Salaam.
Hivyo, tokea siku hiyo, Tume
haikuwa tena na kazi ya kuandaa Ripoti ama Rasimu kwa sababu kazi hiyo
ilikuwa imekwisha na wala isingeweza kuibadili tena Rasimu ya Katiba.
Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka jana, kupitia miezi ya Januari,
Februari mpaka Machi 18, mwaka huu, Sekretariati ilikuwa na muda wa siku
77, zaidi ya miezi unusu, kufanya maandalizi ya kukabidhi nyaraka na
ofisi kwa sababu ilijua kazi yake ilikuwa inamalizika siku ambayo
Mwenyekiti wa Tume hiyo angewasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge
Maalum la Katiba.
Sasa katika muda wote huo,
Sekretarieti ya Tume ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa ripoti ya
makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa
mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike hadharani leo kwa jambo ambalo
lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?
(c) Wajumbe wa Tume kutakiwa kurudisha magari Ikulu
Ni kweli kuwa wajumbe wa Tume
walitakiwa kurudisha Ikulu magari ambayo walikuwa wanatumia kikazi kwa
sababu kazi ya Tume ilikuwa imemalizika.
Pili, Tume ilijua tokea mwanzo
kuwa baada ya kumaliza kazi yao, magari ambayo walikuwa wanatumia
wajumbe na maofisa wa Tume hiyo yalikuwa yanatakiwa kupelekwa Dodoma kwa
matumizi ya shughuli za Bunge Maalum la Katiba ambalo linakabiliwa na
shida kubwa ya usafiri.
Serikali ilichukua uamuzi kuwa
magari hayo yapelekwe Dodoma kwa sababu lisingekuwa jambo la busara kwa
Serikali kutumia fedha za umma kununua magari mengine mapya wakati yale
ya Tume bado yanafaa kufanya kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya
manunuzi ya magari mapya.
Hivyo, ni kweli magari hayo yako
Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka
Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
(d) Wajumbe wa Tume kulipwa kiinua mgongo cha Sh.milioni 200 kila mjumbe
Hakuna shaka kuwa Wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi nzuri sana na wanastahili pongezi
nyingi za wananchi. Lakini kama wanadhani kuwa Serikali ina uwezo wa
kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200 basi
wanajidanganya. Wala wananchi wa Tanzania hawawezi kuelewa maana kabisa
ya malipo hayo makubwa kupindukia.
Alichokizungumza Rais Kikwete
tokea mwanzo wa mchakato ni kwamba atafikiria kuwalipa wajumbe wa Tume
aina fulani ya kifuta jasho ambacho kiwango chake atakiamua yeye na kwa
wakati mwafaka na kulingana na raslimali za Serikali. Mpaka sasa
hajafanya uamuzi juu ya jambo hili.
(e) Posho ya Sh.500,000 kutwa kwa kila mjumbe wa Tume
Ikulu pia inapenda kutoa ufafanuzi
wa habari zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa wajumbe wa
Tume hiyo walikuwa wanalipwa Sh. 500,000 (Laki tano) kama posho ya
vikao kwa siku. Hili nalo siyo la kweli.
Ukweli ni kwamba wajumbe wa Tume
walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho ya vikao kwa siku. Maofisa
waandamizi wa Tume hiyo walikuwa pia wanalipwa posho ya Sh. 200,000
(Laki mbili) kwa siku, maofisa wa kati walikuwa wanalipwa Sh. 150,000
kutwa na maofisa wa ngazi za chini walikuwa wanalipwa Sh. 100,000 kwa
siku kulingana na taratibu za Serikali. Anayetangaza vinginevyo
anajaribu tu kuwapotosha wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
02 Aprili, 2014
Post a Comment