BARAZA la
Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Kidato cha Nne 2015,
yakionesha ufaulu wa watahiniwa wote umeshuka kwa asilimia 0.80,
ikilinganishwa na mwaka 2014 huku zaidi ya asilimia 80 ya watahiniwa
waliofanya mtihani huo wakifeli somo la Hisabati.
Hata
hivyo, asilimia 24 .7 ya watahiniwa wa shule 94.941 waliofaulu wamepata
Daraja la I hadi III, hivyo kuwa na nafasi ya kuendelea na Kidato cha
Tano na watahiniwa 113,489 sawa na asilimia 32 wamefeli mtihani huo.
Katika
matokeo hayo yaliyotangazwa jana Dar es Salaam, wasichana wameshika
nafasi ya kwanza na ya pili katika wanafunzi 10 bora kitaifa, ambao ni
Butogwa Shija wa Canossa ya Dar es Salaam aliyefuatiwa na Congcong Wang
wa Feza Girls pia ya Dar es Salaam.
Akitangaza
matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema
watahiniwa 272,947 kati ya watahiniwa 433,633 wa kujitegemea na shule,
wamefaulu mtihani huo ambao ni wasichana 131,913 na wavulana 141,034.
Akielezea
kwa upande wa watahiniwa wa shule, Dk Msonde alisema watahiniwa 240,996
(asilimia 67.91) ya watahiniwa 384,300 waliofanya mtihani, wamefaulu
mtihani huo. Mwaka 2014, watahiniwa wa shule waliofaulu walikuwa ni
167,643 (asilimia 69.76). Hivyo kwa mwaka huu ufaulu umeshuka kwa
asilimia 1.85.
Alisema
kwa watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 31,951 sawa na
asilimia 64.80. Mwaka 2014 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 29,162 sawa
na asilimia 61.12. Hata hiyo, watahiniwa wa shule 94,941 sawa na
asilimia 24.73 wamepata Daraja la I hadi III huku zaidi ya nusu ya
waliofaulu kwa watahiniwa wa shule 146,055 wakipata Daraja la Nne.
Mwaka
2014 asilimia 30.72 (watahiniwa 73,832) walipata madaraja ya
Distinction, Merit na Credit kwa kutumia mfumo wa Wastani wa Alama
(GPA). Dk Msonde alisema watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa, waliofaulu ni
watahiniwa 7,536 kati ya 16,162.
Kwa mwaka
2014, watahiniwa 6,810 walifaulu. Akizungumzia ufaulu wa masomo kwa
watahiniwa wa shule, alisema masomo ya Civics, Historia, Jiografia,
Kiingereza, Kemia, Baiolojia, Commerce na Book-Keeping, ufaulu wake
umepanda kati ya asilimia 1.09 na 12.86 ikilinganishwa na mwaka 2014.
“Ufaulu
wa juu kabisa ni wa somo la Kiswahili unaoonesha asilimia 77.63 ya
watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu. Ufaulu wa chini
ni somo la Hisabati ambao ni asilimia 16.76. Mwaka 2014 ufaulu ulikuwa
ni asilimia 19.58.” alifafanua bosi huyo wa Necta.
Msonde
aliongeza: “Ufaulu wa masomo mengi upo chini ya asilimia 50, hata idadi
ya watahiniwa waliopata Daraja la I, II na III ni takribani robo ya
watahiniwa waliofanya mtihani hivyo juhudi zinahitajika katika kuinua
kiwango cha ufaulu wa masomo na kuimarika zaidi kwa ubora wa elimu.”
Akizungumzia
upangaji wa shule kwa ubora wa ufaulu, Dk Msonde alizitaja shule 10
bora kuwa ni Kaizirege (Kagera), Alliance Girls (Mwanza), St Francis
Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam), Marian
Boys (Pwani), Alliance Rock Army (Mwanza), Feza Girls na Feza Boys (Dar
es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).
Alizitaja
shule zilizofanya vibaya kuwa ni Pande (Lindi), Igawa (Morogoro),
Korona (Arusha), Sofi (Morogoro), Kurui (Pwani), Patema (Tanga), Saviak
(Dar es Salaam), Gubalk (Dodoma), Kichangani na Malinyi (Morogoro).
Dk Msonde
aliwataja watahiniwa waliofanya vizuri zaidi na shule wanazotoka kwenye
mabano kuwa ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza Girls), Innocent
Lawrence (Feza Boys), Dominick Aidano (Msolwa, Morogoro), Sang’udie
Sang’udie (Ilboru), Asteria Chilambo na Belinda Magere (Canossa),
Humfrey Kimanya (Msolwa), Bright Mwang’onda na Erick Mwang’ingo (Marian
Boys).
Wasichana
Aliwataja
wasichana 10 bora ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza Girls), Asteria
Chilambo na Belinda Magere (Canossa), Lilian Kiwone na Marynas Duduye
(St Francis Girls), Julieth Mbalilaki (Baobao), Vaileth Lazaro
(Kilakala), Nancy Shao (Canossa) na Emmy Shemdangiwa (St Marys Mazinde
Juu).
Wavulana
Aliwataja
wavulana 10 bora ni Innocent Lawrence (Feza Boys), Dominick Aidano
(Morogoro), Sang’udie Sang’udie (Ilboru), Humfrey Kimanya (Msolwa),
Bright Mwang’onda na Erick Mwang’ingo (Marian Boys), Mohamed Kigume
(Marian Boys), David Joseph (Ilboru), Daniel Mabimbi (Alliance Boys),
William Kihanza (Mzumbe).
Aidha, Dk
Msonde alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 87
waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani, kati ya hao 25 ni wa
kujitegemea na 52 ni wa shule na 10 ni watahiniwa na Mtihani wa Maarifa.
Baraza
pia limezuia kutoka matokeo ya watahiniwa 23 wa shule, waliopata
matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya baadhi ya masomo huku watahiniwa
98 walioshindwa kufanya masomo yote, wote watapewa nafasi ya kufanya
mitihani hiyo.
Katika
hatua nyingine, Katibu Mtendaji huyo wa Necta alisema Baraza katika
Mkutano wa 109, wameamua kurejesha utunuku wa mfumo wa madaraja wa Jumla
ya Alama (Divisheni) kuanzia matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2015
kutokana na maoni ya wadau, ambao wameona mfumo wa Divisheni unaeleweka
ukilinganisha na ule wa Wastani wa Alama (GPA) uliokuwa ukitumika awali.
Dk Msonde
alisema kutokana na mabadiliko hayo, alama za ufaulu zitakuwa kama
ifuatavyo; A (alama 75-100), B (65-74), C (45-64), D (30-44) na F (0-29)
wakati wa Kidato cha Sita madaraja yatakuwa A (80-100), B+ (70-79), B
(60-69), C (50-59), D (40-49), S (35-39) na F (0- 34).
Dk Msonde
alisema madaraja ya ufaulu kwa Kidato cha Pili na Nne yatakuwa ni
Daraja la I (pointi 7-17), II (pointi 18-21), III (pointi 22- 25), IV
(pointi 26-33) na Daraja 0 (pointi 34-35) huku wa Kidato cha Sita
itakuwa ni Daraja la I (pointi 3-9), II (pointi 10-12), III (pointi
18-19) na Daraja 0 (pointi 20-21).
CLICK ANY LETTER BELOW TO FILTER CENTRES BY ALPHABET
|
Post a Comment