Danny Welbeck alifunga mabao mawili Alhamisi na kuwawezesha Arsenal kuwalaza miamba wa Italia AC Milan 3-1 na kufuzu kwa robofainali katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.
Mshambuliaji huyo alitamba kwenye siku ambayo aliitwa tena kwenye kikosi cha taifa cha Uingereza.
Arsenal walikuwa wakiongoza 2-0 kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza San Siro lakini walijipata taabani pale Hakan Calhanoglu alipofunga akiwa hatua 30 kutoka kwenye goli baada ya kuwazidi ujanja wakabaji wa Arsenal.
Arsenal walisawazisha upesi, ingawa kupitia mkwaju wa penalti uliogubikwa na utata, baada ya Welbeck kuanguka alipoguswa kidogo na mchezaji Ricardo Rodriguez eneo la hatari.
Alifunga mkwaju huo.
Na baada ya kipa maarufu wa Milan Gianluigi Donnarumma kubwagwa na kombora la mbali la Granit Xhaka, Welbeck alifunga bao la tatu kupitia mpira wa kichwa.
Ushindi huo uliwawezesha Arsenal kufika robofainali katika michuano mikuu ya klabu Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2010.
Watafahamu watakutana na nani robofainali droo itakapofanywa Ijumaa saa 12:00 GMT.
Waliotinga robofainali | |
---|---|
Arsenal, Atletico Madrid, CSKA Moscow, Lazio, Marseille, RB Leipzig, RB Salzburg na Sporting Lisbon. | |
Droo itafanyika Nyon, Uswizi saa 12:00 GMT mnamo Ijumaa |
Ikizingatiwa kwamba Arsenal wamo alama 12 kutoka eneo la kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika Ligi ya Premia, ushindi Europa League inaonekana kuwa njia yao pekee kwa sasa kwao kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Ili kutimiza hilo, watahitaji mabao kutoka kwa Welbeck, ikizingatiwa mchezaji wao waliyemnunua Januari Pierre-Emerick Aubameyang haruhusiwi kucheza msimu huu kwani alishawachezea Borussia Dortmund.
Nini kitafuata?
Arsenal watapumzika wiki mbili kabla ya kurejea dhidi ya Stoke City Ligi ya Premia uwanjani Emirates mnamo 1 April (13:30 GMT).
AC Milan watarudi kusaka ushindi wao wa tano mtawalia wa ligi ya Serie A watakapokuwa wenyeji wa Chievo Jumapili (14:00 GMT).
Post a Comment