0
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) akiwa kwenye picha pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na Viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania alipotembelea ranchi ya Dakawa jana.
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Muhamed Utaly kulia akitoa maelezo ya kuhusu eneo la hekta 20000 zilizoshindwa kuendelezwa na mwekezaji Mtibwa Sugar kwa lengo la ufugaji. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo bwana Stan Rau hapo jana.
Meneja wa ranchi ya Mifugo ya Mkata, Iddi Sadalah akimuonyesha Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) banda la Mbuzi linalokadiriwa kuchukua mbuzi 800 kwa wakati mmoja katika ranchi ya Mkata jana.


……………….

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina ameagiza Mtendaji Mkuu wa Ranchi za Mifugo za Taifa, Profesa Philemoni Wambura kuvunja mikataba ya wawekezaji wa vitalu vyenye jumla ya hekta 68,238 kwenye ranchi ya Mkata na Dakawa ndani ya mwezi mmoja baada kushindwa kuviendeleza vitalu vya ranchi na kushindwa kulipia kwa muda mrefu.Mpina ameyasema hayo jana wakati alipotembelea katika ranchi ya Mkata na Dakawa kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika ranchi hizo.

Amezitaja kampuni za wawekezaji ambazo zilizomilikishwa vitalu zinatakiwa kuvunja mkataba kwa kushindwa kuendeleza upande wa ranchi ya Mkata katika Wilaya ya Kilosa kuwa ni pamoja na Kadolo Farm Company Ltd kitalu namba 418 yenye hekta 4005,Bagamoyo Farm kitalu namba 419 yenye hekta 3672.96, A to Z Animal Feeds Company Ltd kitalu namba 420 yenye hekta 3692.97 na Ereto Livestock Keepers kitalu namba 422 yenye hekta 4020.54.

Katika Wilaya ya Mvomero kampuni zilizoshindwa kuendeleza vitalu ni pamoja na kampuni ya Overland kitalu namba 415 yenye hekta19446.28, Katenda yenye hekta 2500, Mollel yenye hekta 2500 na Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa (Mtibwa Sugar) chenye hekta 20000 walizomilikishwa toka mwaka 1999 na kushindwa kukiendeleza na kukilipia kwa miaka 18.

Mpina amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kumaliza mara moja migogoro inayoendelea baina ya wakulima na wafugaji. Aidha Waziri Mpina amemtaka Diwani wa kata yaTwatwatwa, Katibu Tawala wa Halimashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na jamii ya wafugaji kumaliza migogoro inayowasumbua kwa muda mrefu kwa njia ya mazungumzo kabla ya kukimbilia muhimili wa mahakama bila sababu yoyote.

Mpina amesema kama vyombo vya Serikali vingetumika vizuri kuanzia ngazi ya kijiji kungepunguza migogoro ya wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo. Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa Wilaya zinaongoza kwa kuwa na migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

Kwa upande mwingine, Waziri Mpina amezitaka Halimashauri zote nchini kutotunga sheria kandamizi dhidi ya wafugaji. Akitolea mfano, wa sheria ndogo ya Halimashauri ya Mvomero ya kutoza faini ya shilingi 25, 000/=kwa kila mfugo kuingia katika Wilaya hiyo bila kufuata taratibu badala ya shilingi elfu kumi iliyoelekezwa katika Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya Mwaka 2003.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Magembe Makoye amesema upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wafugaji kutasaidia kuondoa migogoro baina ya pande hizo na kuendelezwa kwa ranchi hizo za taifa kutawasaidia wafugaji kupata shamba darasa litakalo wasaidia kufuga kwa kisasa na kupata mbegu bora za mifugo.

Post a Comment

 
Top