0

Nahodha na beki mkongwe wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, yupo kwenye mazungumzo ya mwisho na klabu yake hiyo ya kuongeza mkataba mwingine wa miaka miwili.

Beki huyo alijiunga na Yanga kwenye msimu wa 2006/07 akitokea Zanzibar alipokuwa anacheza soka kabla ya kutua Jangwani.

Cannavaro tangu ajiunge na Yanga hajaihama timu hiyo hadi hivi sasa huku akifanikiwa kubeba makombe matatu ya Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii mbili na Kombe la FA mara moja na Kombe la Chalenji akinyanyua mara moja.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Cannavaro alisema wakati wowote anatarajiwa kusaini mkataba mara baada ya kufikia makubaliano mazuri na viongozi wa timu hiyo.

Cannavaro alisema anaamini miaka miwili hiyo ndiyo ya mwisho kwake kuendelea kucheza soka ambayo mara baada ya kumalizika, basi atatangaza rasmi kustaafu.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kustaafu soka, haraka ataanza kozi ya ukocha ili baadaye katika maisha yake awe kocha.

“Mimi nina miaka yangu miwili ya kucheza soka pekee na badala yake nitawaachia wachezaji wengine vijana ili wapate nafasi ya kuonekana katika soka.

“Hivyo, hivi sasa nipo mimi nipo kwenye mazungumzo na mabosi wangu wa Yanga kwa ajili ya kuongeza miaka miwili ya mwisho,” alisema Cannavaro.

Post a Comment

 
Top