Naibu Waziri Mgalu Awataka Wakandarasi Tanga kutoa Maelezo Ya kutokuanza Miradi
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo mbele ya wanakijiji wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto mbele) akiendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo kwa wakazi wa kijiji cha Magumbani kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Mkazi wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga, Mohamed Mengwena akitoa pongezi kwa Serikali kwa kufikisha miundombinu ya umeme kijijini hapo mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo tarehe 16 Desemba, 2017.
Msimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA) katika mkoa wa Tanga, Mhandisi Kasim Rajabu akieleza jambo mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, na wakazi wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na serikali wakisikiliza kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wanakijiji wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Na Greyson Mwase, Tanga
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezitaka kampuni za Derm Electric, Njarita, Agwilla na Radi Services kutoa maelezo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kutokuendelea na kazi katika maeneo yao ya miradi wakati walikwishalipwa malipo ya awali na Serikali.
Mgalu alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki tarehe 16 Desemba, 2017 alipofanya kikao na watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)- Ofisi ya Tanga baada ya kubaini wakandarasi hao hawapo katika maeneo hayo ya kazi na kutohudhuria kikao hicho kama alivyoagiza.
Kikao hicho kilishirikisha pia watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Alisema kitendo cha wakandarasi kutokuwepo katika maeneo yao ya kazi na kutohudhuria kikao kama ilivyoagizwa kinakwamisha utekelezaji wa miradi na hivyo kuutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kujulisha kampuni husika kuandika maelezo ya kutokuwepo kwenye maeneo ya kazi na kukwamisha juhudi za Serikali katika usambazaji wa umeme vijijini.
“ Kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2019- 2021 vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme, sasa inapotokea baadhi ya wakandarasi wanakwamisha juhudi hizi wakati wamekwishalipwa na Serikali ni lazima Serikali iwawajibishe kulingana na sheria na kanuni za nchi,” alisema Mgalu.
Mgalu aliendelea kuwataka wakandarasi wote nchini kuwepo katika maeneo yao ya kazi na kukamilisha miradi yao kwa wakati, na kusisitiza kuwa serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi katika kiwango cha chini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliitaka TANESCO kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa madeni na kukamilisha zoezi la uhakiki wa wateja mara moja ili kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mapato ya shirika hilo.
Alisema ni jukumu la TANESCO kujiendesha kwa faida kupitia mapato yake na kazi ya Serikali ni kulipa nguvu shirika hilo kwa miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi.
Wakati huo huo, akizungumza katika mikutano tofauti katika kijiji cha Zangibari kilichopo wilayani Mkinga na katika vijiji vya Mlingano, Mtindiro, Mpapayu vilivyopo katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Naibu Waziri Mgalu alielekeza wakati wa utekelezaji wa miradi, Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuhakikisha taasisi, shule, nyumba za ibada, hospitali zinapata umeme.
Aidha alipongeza wananchi wengi katika vijiji vya Zangibari wilayani Mkinga na Mpapayu wilayani Muheza mkoani Tanga walioonyesha mwitikio mkubwa wa kuunganisha mfumo wa umeme ( wiring) kwenye nyumba zao na kuwataka ambao hawajaunganisha mfumo wa umeme kufanya mara moja kwa ajili ya neema kubwa ya umeme.
Alisema kwa wale ambao wana nyumba ndogo wanaweza kuwekewa kifaa maalum cha Umeme Tayari (UMETA) na kuanza kufaidi huduma ya umeme.
Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vyote vitakuwa na umeme wa uhakika.
Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.
Post a Comment