Kaimu Kamishna wa Polisi, Juma Yussuf Ali
****
JESHI la Polisi Zanzibar limeanza kufanya uchunguzi baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara Naushad Mohamed Suleiman akiwa na kilo nane za dhahabu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Kaimu Kamishna wa Polisi Juma Yussuf Ali, alisema mfanyabiashara huyo aliyekuwa mfadhili wa mashindano ya soka na timu ya Malindi Zanzibar, alikamatwa baada ya jeshi hilo kupatiwa taarifa kuhusu kubeba almasi hiyo.
“Tumeanza uchunguzi ili kujiridhisha kama kweli mtuhumiwa anamiliki almasi hizo au tuanze mchakato wa kumshtaki,” alisema Kamishna huyo na kuongeza kuwa kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo ni jitihada za jeshi hilo za kuhakikisha rasilimali za Tanzania zinalindwa.
Mtuhumiwa huyo alikuwa na kilo nane za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani milioni 746.89 kulingana na bei ya sasa ya dhahabu, ambayo ni dola za Marekani 41,564.45 kwa kilo pamoja na aina fedha za aina mbalimbali kutoka nchi 15 duniani.
Mfanyabiashara huyo alikuwa anajiandaa kusafiri kwa ndege ya FlyDubai majira ya saa tatu usiku akienda Dubai.
Rais John Magufuli hivi karibuni alianzisha hamasa ya kupambana na ufisadi, rushwa na wizi wa kimataifa wa rasilimali za Tanzania. Agosti 31, mwaka huu, Mamlaka za Tanzania Bara zilikamata almasi zenye thamani ya dola za Marekani milioni 15 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, zilizokuwa zikisafirishwa kupelekwa Antwerp, Ubelgiji.
Almasi hizo zilikuwa zikisafirishwa kampuni ya uchimbaji madini ya Williamson Diamonds, inayomilikiwa na raia wa Uingereza, Petra. Katika muendelezo wa uchunguzi wa tukio hilo, maofisa wawili wa serikali walishtakiwa kwa uhujumu uchumi.
Maofisa hao ambao ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Tathmini ya madini ya almasi cha taifa, Archard Kalugendo na Mtathmini wa almasi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, walishtakiwa kwa kufanyia almasi hizo tathmini ya na kusababisha serikali kupata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.1 sawa na Sh bilioni 2.5.
Wakati huohuo, Kamishna huyo wa Polisi alibainisha kuwa kiwango cha uhalifu ikiwemo mauaji visiwani Zanzibari, kimepungua kutoka mauaji ya watu 34 mwaka jana hadi kufikia 24 mwaka huu.
Alisema mafanikio hayo yametokana na jeshi hilo, kuongeza ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali visiwani humo. Aidha, alisema matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, pia yamepungua kutokana na ushirikiano baina yao na serikali kuongezeka. Hata hivyo, alieleza kuwa unyanyasaji wa majumbani na wizi katika makazi ya watu, kama vile mazao ya shambani na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana bado ni matatizo, ambayo polisi wanaendelea kuyafanyia kazi.
Chanzo-Habarileo
Post a Comment