0


Huenda ikawa kesho asubuhi umepanga kula mkate na chai au ukasindikiza kitafunwa hicho na chochote kile na inawezekana pia  ikawa mkate ndio kitafunwa chako kikuu kila lichomozapo jua. Je, una habari kuwa ni hatari kwa afya yako?

Utakubaliana na mimi kwamba, Mkate ndiyo chakula kikuu cha kila siku cha familia nyingi duniani, hasa sehemu za mijini na ndiyo chakula kinachotumika na watu wa rika zote, wakubwa kwa wadogo, lakini ni wangapi tunajua kuwa
mkate mweupe, ambao ndiyo chaguo namba moja la familia nyingi, ni hatari kwa afya zetu?

Hebu nikukumbushe msemo wa maarufu wa Kiingereza kuhusu mkate mweupe usemao 'The Whiter the Bread, the Quicker You are Dead!' kwa tafsiri isiyo rasmi, msemo huu unamaanisha kuwa ‘Kadiri unavyopenda kula mkate mweupe, ndivyo utakavyokufa haraka!’ Amini, usiamini, mkate mweupe siyo mzuri kwa afya yako!

Inawezekana kabisa habari hii isikufurahishe, lakini kama kweli unataka kuboresha afya yako, unapambana na suala la kupunguza unene, unataka kujiepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari , ugonjwa wa moyo au saratani ya tumbo, basi huna budi ya kuachana na mkate mweupe.

Inafahamika kuwa vyakula vyote vitokanavyo na nafaka zilizokobolewa vina hasara zaidi kiafya kuliko faida, mkate mweupe nao ni miongoni mwa vyakula hivyo.

Kwa nini usile mkate mweupe?
Kama ujuavyo, mkate unatengenezwa kutokana na ngano na mkate mweupe unatokana na unga wa ngano iliyokobolewa na kuondolewa virutubisho vyake muhimu vya asili ambavyo huwa muhimu katika uimarishaji wa mfumo wa usagaji na umeng’enyaji chakula tumboni yaani kwa lugha ya kitaalam Digestive system and metabolism.

Ili unga uwe mweupe, ngano baada ya kukobolewa husafishwa kwa mashine maalum kwa kutumia kemikali na joto kali, kitendo ambacho huondoa kabisa virutubisho vinavyoweza kuwemo kwenye nafaka na hivyo kuiacha punje ya ngano ikiwa nyeupe na kubaki makapi.

Makapi hayo, baadaye husagwa na kuwa unga safi na mweupe ambao hutayarishwa kabla ya kutengenezwa mkate kwa kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo hatua ya kuwekewa hamira ili uumuke, kuongezewa sukari pamoja na chumvi ili kuongeza ladha.

Madhara unayoweza kupata kwa kula mkate mweupe?
Madhara ya kwanza unayoweza kuyapata kwa kupenda sana kula mkate mweupe ni ugonjwa wa kisukari.

Utafiti unaonesha kuwa mkate au chakula chochote kilichotengenezwa kutokana na unga mweupe kina kiasi kingi cha wanga ambao husababisha kuongezeka sukari mwilini.

Madhara mengine yatokanayo na mkate mweupe ni kuongezeka kwa lehemu yaani 'cholesterol' kwenye damu, hali ambayo inaweza kusababisha presha au magonjwa ya moyo yatokanayo na kusinyaa au kuziba kwa mishipa ya damu.

Madhara hayajaishia hapo, mengine yanayoweza kukupata ni tatizo la ukosefu wa choo kwa muda mrefu.

Mkate mweupe huchangia kuvuruga mfumo wa umeng’enyaji wa chakula tumboni yaani 'metabolism system'.
Mwili unapokuwa hauna virutubisho vya kutosha, usagaji na uondoaji wa sumu mwilini huwa wa shida na uchafu unaporundikana tumboni kwa muda mrefu bila kutoka, husababisha kansa ya tumbo!

Je, ule nini badala ya mkate mweupe? 

Kuna aina nyingine ya mkate ambayo ndiyo unayopaswa kula, mkate huo ni 'brown bread'  au kwa jina   maarufu la hapa nchini kwetu kwa wale wenangu na mimi huita 'mkate mweusi'.

Mkate huu hutengenezwa kutokana na ngano isiyokobolewa hivyo kuwa na virutubisho vyake asilia vinavyohitajika mwilini na kuwa na faida zitakazokuepusha na kupatwa na madhara yaliyotajwa hapo juu.

Mkate huu hauna sukari wala chumvi, hivyo kuwa bora zaidi kwa afya yako.

Afya ya mtu hujengwa na mtu mwenyewe au upo tayari kujichimbia kaburi lako mwenyewe? Kama jibu ni hapa anza kula mkate mweusi badala ya mweupe kuanzia leo.
Brown bread au Mkate mweusi

Post a Comment

 
Top