0

Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki inamwezesha mfugaji kuongeza uzalishaji pamoja na kipato.

 Chumba cha nyuki 1Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwepo na kudumu kwa karne nyingi sana. Shughuli ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania hasa katika mkoa wa Tabora ambao ni maarufu kwa uzalishaji wa asali, ilianza kutambulika rasmi tangu mwaka 1884, wakoloni kama vile Rebman na Craft walipofika katika eneo hilo.

Katika kipindi hicho, jamii ya eneo hilo walikuwa wanafuga nyuki kwenye magome ya miti, vibuyu, vyungu, mapango, vichuguu na kwenye miamba. Baada ya muda ufugaji ulipiga hatua kidogo na watu wengi wakawa wanafuga kwa kutumia mizinga iliyochongwa kutoka kwenye magogo ya miti. Ufugaji wa aina hii umedumu kwa karne nyingi kote nchini Tanzania.

Kutokana na uhitaji na ongezeko la matumizi ya bidhaa za nyuki, kulifanyika tafiti mbalimbali ambazo ziliweza kuboresha ufugaji wa nyuki kwa kuwa na mizinga ya kisasa ambayo imewezesha uzalishaji wa asali kuwa mkubwa na kuongeza pato la wafugaji tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Tafiti hazikuishia kwenye kuboresha mizinga tu, ila siku hadi siku kunavumbuliwa namna bora zaidi za kuimarisha uzalishaji wa nyuki. Katika makala hii, tutazungumzia namna ambavyo unaweza kuwajengea nyuki nyumba ili kuboresha mazingira yao ya uzalishaji, na hatimae kupata ufanisi zaidi.

Nyumba ya nyuki
Hii ni aina mpya ya ufugaji wa nyuki ambapo unaweza kujenga kibanda au nyumba kisha kuweka mizinga idadi unayohitaji.

Ni kwa nini kujenga nyumba au kibanda?
• Ni muhimu kufuga nyuki kwenye kibanda au kwenye nyumba kwa sababu inasaidia kudhibiti wizi wa mizinga, pamoja na wanyama wanaokula asali na kudhuru nyuki.
 • Inarahisisha utunzaji wa mizinga na kuwafanya nyuki wasihame kwenda sehemu nyingine.
• Inasaidia watu wengi kujifunza namna nzuri ya ufugaji wa nyuki, ikiwa ni pamoja na watoto, jambo ambalo linafanya shughuli hii kuwa endelevu.
• Ufugaji wa aina hii unasaidia kuwak inga nyuki dhidi ya majanga kama vile moto, na mafuriko.
• Inawaepusha nyuki na usumbufu unaoweza kuwafanya wasizalishe kwa kiwango kinachotakiwa.
• Uzalishaji unaongezeka. Hii ni kwa sababu mizinga inayotumika ni ile ya kibiashara. Mzinga 1 unapata asali kilo 30 sawa na lita 20.

Chumba cha nyukiAina ya nyumba
Unaweza kujenga nyumba yenye upana wa futi 3 na urefu wa futi 9. Nyumba hii inaweza kuchukua mizinga hamsini. Halikadhalika, unaweza kujenga kibanda chenye ukubwa sawa na huo.

Eneo linalofaa
• Ili kuwa na ufanisi mzuri, nyumba hii inafaa kujengwa nje kidogo ya makazi ya watu.
• Kusiwe na mifugo karibu.
•Iwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufika.
• Isiwe karibu na njia ambayo watu wanapita mara kwa mara.
• Kusiwe na aina ya mimea ambayo nyuki hawapendi.
• Kuwe na maji karibu.

Mavuno
Baada ya kujenga nyumba, kuweka mizinga na nyuki kuingia, unaweza kuvuna kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu. Utaweza kupata mavuno mazuri endapo utavuna kabla nyuki na wadudu wengine hawajaanza kula asali.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa wadudu waharibifu kama vile sisimizi, mende na wengineo wanadhibitiwa ili kutokuathiri uzalishaji wa asali. Hakikisha unavuna kitaalamu ili kuepuka upotevu wa asali. Endapo nyuki wametunzwa vizuri na kwenye mazingira mazuri, unaweza kuvuna asali mara tatu kwa mwaka. Katika mzinga mpya nyuki wana uwezo wa kutengeneza masega kwa siku tatu na kuanza uzalishaji wa asali.

Ni nini umuhimu wa asali
• Asali inatumika kama chakula
• Inatumika kama tiba ya magonjwa mbalimbali
• Hutumika kutibu majeraha
• Ni chanzo kizuri cha kipato
• Hutumika katika kutengeneza dawa za binadamu
*Asali inaweza kuhifadhiwa kwa miaka mingi sana bila kuharibika. Hii inatokana na wingi wa dawa maalum iliyo nayo inayofanya isiharibike.


Bidhaa zinazotokana na asali
 Chumba cha nyuki 2Kuna aina nyingi ya bidhaa zinatokana na asali, kwa kutengenezwa na nyuki wenyewe na nyingine zikitengenezwa na binadamu kutokana na tafiti mbalimbali. 

Miongoni mwa bidhaa hizo ni:
• Asali yenyewe
• Royal jelly : Hii ni aina ya maziwa yanayotengenezwa na nyuki, ambayo hutumika kama tiba.
• Gundi: Hii hutumika kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtumiaji.
• Nta: hutumika kutengenezea mishu maa, kulainisha nyuzi, kutengeneza dawa ya viatu, mafuta ya            kupaka, pamoja na dawa ya ngozi.

Post a Comment

 
Top