0
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imeanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha kama ambavyo ilikabidhiwa jukumu hilo kuanzia mwezi Julai kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017.


Hayo yameelezwa jana septemba 13  jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa kodi katika michezo hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Aidha ametaja maeneo ambayo  TRA inakusanya mapato katika michezo mbalimbali ya kubahatisha kuwa ni kama Casino, Sport Betting, Slot Machines, Lottery na kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) na kusisitiza kuwa kiwango cha kodi kinatofautiana kati ya mchezo mmoja na mwingine.

“Jukumu hili limetokana na mabadiliko ya sheria ambayo yapo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 ambayo imetupa mamlaka kamili ya kusimamia zoezi la ukusanyaji wa mapato katika michezo ya kubahatisha,” ameeleza Kayombo.

Amefafanua kwamba wanaojihusisha na michezo hiyo katika Casino wanapaswa kuwasilisha TRA asilimia 15 ya mapato yanayotokana na mchezo huo kwa wiki huku wanaochezesha michezo ya Sport Betting wakitakiwa kuwasilisha asilimia 6.

Kayombo ameongeza kuwa kwa wale ambao wanaochezesha michezo hiyo kwa njia ya SMS watatakiwa kuwasilisha asimilia 30, kwa michezo ya kitaifa (National Lottery) wanatakiwa kuwasilisha asilimia 10 na michezo ya slot machine wanatakiwa kuwasilisha sh. 32,000 kwa mwezi kwa kila machine moja. 

“Michezo ya kubahatisha ina pande mbili yaani mchezeshaji na mchezaji hivyo kila mmoja anapaswa kulipa kodi, ambapo mshindi wa mchezo huo pia anapaswa kulipa asilimia 18 ya mapato yake ambayo hukatwa na mchezeshaji na kuiwasilisha TRA,” alisema Kayombo.

Aidha Kayombo amesisitiza kuwa TRA itajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato tu, jukumu la kuratibu na kuendesha michezo hiyo litabakia kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha hapa nchini ambayo ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia michezo yote ya kubahatisha.

Amesema TRA inashirikiana na Bodi ya Michezo hiyo katika kutoa elimu kwa wadau wote wanaohusika na michezo ya kubahatisha wakiwemo wadhamini, wananchi, vyombo vya habari na wadau wengine.

Post a Comment

 
Top