0

Siku moja ikiwa ni miaka mingi ya nyuma iliyopita, palitokea ndugu wawili waliokuwa marafiki waliopata nafasi ya kutembelea nchini India kwa kufanya utalii nchini humo. Walipokuwa wakitembea katika mitaa mbalimbali ya mji wa Bombay walishangaa sana kuona maelfu ya watu waliokuwa masikini wamezagaa na kukaa kila kona ya njia za mitaa ya mji huo. Baadhi ya watu walionekana wamekaa chini ya madaraja na mabakuli ya kuombea msaada, na wengi wao zaidi wakizunguka katika mitaa hiyo huku wakionekana ni watu wasiojiweza kabisa (masikini sana) tena wakiwa pekupeku pasipo kuvaa viatu.

Mmoja wa wale marafiki wawili waliokuwa wakitembea pamoja akamwambia mwenzake, “angalia hao watu. Wanatia huzuni sana?” Wanatembea bila viatu. Na tena ni watu wengi (maelfu ya watu). Hii inatia huruma sana. Na pia ni aibu kubwa kwa taifa kama letu tulikotoka ambako kuna kila aina ya viatu vingi vya kuweza kuwasaidia hawa watu tunaowaona huku wakitembea pasipo viatu. Sitasahau jambo hili nililoliona kwa macho yangu kwani linatia huruma. Akamalizia kwa kusema, “nitakaporudi nyumbani (nchini mwake) nitamsimulia mke wangu kuhusu kisa hiki nilichokiona.” Ndugu huyu aliendelea kuongea mambo mengi kuhusu namna alivyoona masikini wanavyotembea pekupeku pasipo viatu miguuni mwao.

Kwa muda huo yule rafiki yake alikuwa ameamua kuchukua kipande cha karatasi na akaweza kuandika mambo baadhi aliyokuwa ameyaona katika mji ule. Baada ya hapo alivyorudi nchini mwake Marekani moja kwa moja alianza kufatilia kwa karibu mkakati ule aliouandika na namna gani atakavyoweza kusafirisha viatu kutoka nchini mwake kupeleka nchini India, na namna gani ya kuweza kutengeneza kiwanda na kuzalisha viatu moja kwa moja akiwa huko huko nchini India.

“Ukiona Mungu ameruhusu uone tatizo lililoko kwenye mazingira yaliyokuzunguka ujue ameona unao uwezo mkubwa ndani yako aliouweka wa kuitua changamoto hiyo.” -Wilfred Tarimo

Hebu tazama tofauti ya watu hawa wawili, wa kwanza anawaza na kusema, “angalia watu hawa wanavyotembea peku peku pasipo kuvaa viatu na kisha kuwaonea huruma tu,” Huyu wa pili yeye aliamua kusema, “nikitazama hawa watu miguuni ni wazi kabisa wanahitaji viatu.” Hii ni wazi wote wawili walikuwa na macho ya kuona changamoto na tatizo lile lakini ni wazi pia kila mmoja aliona na kuchukulia changamoto Ile kwa namna ya tofauti. Mmoja aliona ni tatizo kama tatizo na kuishia kuwaonea huruma watu wale, mwingine aliona changamoto kama FURSA ya kutatua ili kuwasaidia watu wale wa mji wa Bombay na zaidi sana kwa kupitia changamoto ile, yeye aweze kufanikisha maono ya kile alichokuwa anakiona ndani yake.

Leo hii ndugu huyu ameweza kufungua biashara kubwa na kuwa na kampuni mojawapo kubwa inayohusika na uzalishaji wa viatu nchini Marekani. Mmoja aliona miguu isiyo na viatu na kubaki kuongea pasipo kuchukua hatua yoyote kivitendo. Na mwingine aliona fursa ya kibiashara kupitia miguu isiyokuwa na viatu. Hii ni wazi kabisa tukisema, Maisha ni vile unavyowaza na kuona ndani yako na hapo ndivyo utakavyofanikiwa. Ni wazi ukiwa mwenye Maono makubwa ndani yako ukaunganisha na Imani ndogo uliyonayo, utaona kila changamoto unayokutana nayo kama fursa ya kipekee ya kukusaidia kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine na si kikwazo cha kukukwamisha mahali ulipo.

Ili ufanikiwe kwenye maisha yako unahitaji kuona changamoto unazokutana nazo kila mara kama fursa iliyoficha utajiri mwingi ndani yake na si kuishia kuongelea na kuikimbia changamoto yenyewe.  Ukiona Mungu ameruhusu uone tatizo lililoko kwenye mazingira yaliyokuzunguka ujue ameona unao uwezo mkubwa ndani yako aliouweka wa kuitua changamoto hiyo. Ile kuishi duniani tu, unapaswa kutambua bado Mungu anataka ujifunze kuona changamoto kama fursa unazotakiwa kuzitatua. Moja ya sababu iliyotuleta duniani kuishi, ni kutatua changamoto ili kuleta majibu kwa watu na dunia tunayokaa. Amini unauwezo mkubwa wa kufanya makubwa kuzidi yale yaliyokwisha kufanyika hapo nyuma.

Post a Comment

 
Top