0
WANAFUNZI 33, walimu wawili na dereva waliokuwa walevi mnamo Ijumaa walilala ndani ya seli katika Kituo cha Polisi cha Ol Kalou, Nyandarua. 
Wanafunzi hao wote walikuwa wa kidato cha nne katika shule ya mseto ya Naivasha, Kaunti ya Nakuru. 
Walikamatwa Ijumaa saa tatu usiku ndani ya klabu moja kinachomilikiwa na duka la reja reja Ol Kalou.
Polisi walipata aina tofauti za vileo na vinywaji kama soda vilivyokuwa vimechanganywa na vileo. Walikuwa ni pamoja na wasichana 11, vijana 22 na walimu wawili wa miaka 24 na 27.
Katika kituo cha polisi, maafisa wa polisi walikuwa na wakati mgumu kuwadhibiti wanafunzi hao walioonekana walevi.
“Baadhi ya wasichana walionekana uchi, inaonekana kuwa walikunywa siku yot. Hawakujua kwamba wamekamatwa. Waliimba na kucheza densi za mugithi ndani ya kituo cha polisi,” alisema afisa wa polisi.
Alisema baadhi ya wasichana walionekana kuwaalika watu wasiowajua kujiburudisha.
Msimamizi wa polisi eneo hilo Wilson Kosgei alisema polisi walifuata gari lao kutoka mjini Nyahururu walipodokezewa na wananchi kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa vibaya na wanafunzi walikuwa wakijihusisha na tabia mbaya.
“Walikuwa katika ziara ya Nakuru na baadaye Nyahururu. Waendeshaji wa magari katika barabara ya Ol Kalou kuelekea Nyahururu walilalamika kuwa gari lao lilikuwa likiendeshwa vibaya na wanafunzi walionekana kuwa na tabia mbaya,” alisema msimamizi huyo.
Baada ya kufika Ol Kalou, hawakuwa wakijua walikuwa wakifuatwa na polisi, basi hilo lilisimama karibu na duka hilo ambapo walimu na wanafunzi walinunua vileo zaidi.

Post a Comment

 
Top