RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesisitiza azma ya Serikali ya
kuwaongeza mshahara wafanyakazi wa kima cha chini ifikapo Aprili mwaka huu kuwa
iko pale pale.
Akifunga semina ya siku moja kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Takwimu na Matumizi yake, katika ukumbi
wa Baraza la wawakilishi la zamani, Dkt. Shein amesisitiza kuwa Serikali ipo
vizuri na kueleza kuwa ahadi zote zitatekelezwa sambamba na vikosi vya SMZ
kulingana kimaslahi na vikosi vyengine.
Pamoja na hayo Dkt. Shein amesisitiza kauli yake kuwataka viongozi na
watendaji katika sekta ya umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea amesema kuwa ni
jukumu la kila kiongozi kubadilika katika utendaji wake wa kazi.
Dkt. Shein amesema tangu alipoingia madarakani mwaka 2010 Zanzibar imepiga
hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato na kuchangia kuongezeka takriban mara
nne.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesisitiza haja
ya kuwepo kwa mashirikiano katika utoaji wa takwimu na kuzitaka taasisi za umma
na zile binafsi kushirikiana vyema na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Asema kuwa takwimu zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi pamoja na
wananchi wake na zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanya maamuzi,
kuwahudumia wananchi pamoja na kuzisaidia Wizara katika kutekeleza mipango
yake.
Semina hiyo ilikuja na maazimio ambayo yalisomwa mbele ya washiriki wote
kufuatia mada tano silizowasilishwa na wasilishaji mbali mbali kutoka Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Serikali zenye maudhui tofauti ikiwemo mada ya Muhtasari wa
majukumu ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika upatikanaji wa takwimu na
matumizi yake.
Mada nyengine ilikuwa ni Umuhimu wa takwimu, hatua za uzalishaji na
matumizi yake, Takwimu za sekta ya kilimo, Takwimu za sekta ya viwanda na
Takwimu za sekta ya huduma.

Post a Comment