Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais, Dkt. John Magufuli
hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu
swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe
katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt.
Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya
upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua nini
kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini,
Mheshimiwa Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi huyo alitaka kujua
kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo, Mheshimiwa Peter Lijualikali
pamoja na madiwani sita wa chama hicho ambao wamefungwa na viongozi wengine 215
wanaokabiliwa na kesi mbalimbali.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa nchi inaendeshwa katika mihimili
mitatu ikiwemo Serikali, Mahakama na Bunge na kwamba hakuna muhimili unaoweza
kuuingilia muhimili mwingine.
Amefahamisha kuwa Watanzania wanajua
kwamba jambo lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali pengine
popote, hivyo hawezi kuzungumzia mambo yote yanayoendelea chini ya sheria na
yaliyo mahakamani kutumia bunge.
Wakati huo huo;
Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari
halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea kuzalisha na hadi
mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.

Post a Comment