
OFISA Mtendaji wa Kata ya Mgongo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida,
Mwajuma Rugambwa (42), amejeruhiwa na fisi aliyemvamia, ambaye
alipambana naye ili kunusuru uhai wake.
Tukio hilo lilitokea juzi baada ya mtendaji huyo akiwa kazini kupigiwa
simu na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgongo, Humphrey Mkumbo kuhusu uwepo wa
fisi huyo ambaye alijeruhi wananchi wawili ambao hadi sasa wanaendelea
na matibabu katika hospitali ya wilaya.
Akisimulia tukio hilo wakati akizungumza na MTANZANIA, Mwajuma alisema
baada ya kupata taarifa ya uwepo wa tukio hilo, alipiga kipyenga cha
kuashiria hali ya hatari na wananchi walikusanyika ili kuweza kumsaka
fisi huyo.
Alisema wakati akiendelea na kazi hiyo, kumbe fisi alikuwa amejificha
juu ya mbuyu na ghafla alishuka na kuanza kumrarua mwilini, lakini
alipambana naye na kufanikiwa kumdhibiti.
“Nilipopata taarifa hiyo nilichukua hatua ya kupiga kipyenga ili
kuashiria kuna tukio la hatari. Wananchi walikusanyika kwa ajili ya
kumsaka fisi huyo ambaye alikuwa amejificha kwenye pango la mti wa
mbuyu.
“Kwa kuwa tulikuwa tumetawanyika kidogo, nilimuona fisi ametoka mbio na
akaanza kumrarua kijana mmoja ambaye sikufahamu jina lake haraka, na
mimi nikiwa na jiwe na mkoba wangu, aliponiona akaanza kunirarua na
akaniangusha chini.
“Baada ya kuniangusha akaniuma paja la kulia, ghafla ujasiri ulinijia na
kumkaba koo kwa mikono yote miwili, nilipomkaba akaniuma mkono wa
kushoto hadi kidole kimoja kikavunjika.
“Hata hivyo sikuachilia mkono wa kulia, nilizidi kumkaba koo hadi
wananchi walipokuja kunisaidia na kumuua,’’ alisema Mwajuma huku
akiugulia maumivu makali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi, Dk. Adam
Mashenene, alisema juzi saa mbili asubuhi walipokea majeruhi wawili
walioshambuliwa na fisi kutoka katika Kijiji cha Mgongo.
“Majeruhi hao ni Masunga Ngusa (29) na Nkomba Ngusa (27), ambao
walifikishwa hapa hospitali kwa matibabu na tuliwaingiza katika chumba
cha upasuaji kuwafanyia huduma ya kwanza kwa kuwasafisha ili kuondoa
uchafu katika vidonda ambavyo fisi huyo alikuwa akinyofoa kula nyama
katika sehemu za miili yao na majeruhi mwingine alivunjwa mkono,”
alisema Dk. Mashenene.
Alisema kwa kuwa hospitali yao haina uwezo wa kutibu majeraha hasa
kufanya upasuaji mkubwa, waliwapa rufaa na kuwapeleka katika Hospitali
ya Misheni ya Hydom, Mkoa wa Manyara kwa matibabu zaidi.
Dk. Mashenene alisema kutokana na tukio hilo, ilipofika saa tisa alasiri
walipelekwa majeruhi wengine hospitalini hapo ambao walijeruhiwa na
fisi huyo ambao ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mgongo, aliyeumwa paja la
kulia na mkono wa kushoto na kusababisha kidole kuvunjika na mwingine
aliyeshambuliwa mkono wa kushoto ambao hadi sasa bado wanaendelea na
matibau hospitalini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, aliwatembelea majeruhi hao
na kuwapa pole, huku akiwapongeza kutokana na ujasiri wa kupambana na
fisi huyo, hasa Ofisi Mtendaji Mwajuma.
Na Seif Takaza-Mtanzania Singida
Post a Comment