Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali
kutangaza rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na hali ya
chakula kuwa mbaya nchini.
Kauli ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisisitiza
utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea.
Agizo la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya Waziri wa Kilimo,
Dk Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya chakula ambapo
Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge huyo wa
Kigoma Mjini akisema ni mbaya.
Jana, mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea
udiwani Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli yake
akisema, “Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”
Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala ya Taifa na
kujionea hali ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.
“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua muhimu ya kisheria ya kutangaza
baa la njaa nchini. Tamko la baa la njaa litaisaidia Serikali kupata
bajeti ya dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya
kutangaza bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema Zitto huku
akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.
Post a Comment