POLISI
Kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kitaanza kukamata magari yote
ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa
taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.
Uwekaji
wa taa hizo zenye mwanga mkali, umezuka kwa kasi katika maeneo
mbalimbali nchini, jambo ambalo limetajwa linaweza kusababisha ajali kwa
dereva atakayemulikwa na taa hizo.
Kauli
hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi hicho, Naibu Kamisha Mohammed
Mpinga ofisi kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema ukamataji wa
magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.
Mpinga
alisema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani,
kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo
yamewekwa taa hizo.
“Ziko
taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku
utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi
ambacho zimeleta matatizo kwa madereva wengine,”alisema Kamanda Mpinga.
Aidha,
alisema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa,
kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi
ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti
chombo chake.
Kamanda
Mpinga alisema kuwa walishatoa muda wa kutosha kwa wamiliki wote wa
magari, walioweka taa hizo kuziondoa, hivyo kwa sasa wataanza
kuwachukulia hatua wote ambao watakuwa hawajaziondoa.
Alifafanua
kuwa uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani
Kifungu cha 39 Sura ya 168, ambacho kinaeleza matumizi ya taa. Mpinga
pia alisema magari yatakayokamatwa ni yale ambayo yameongezewa taa hizo.
Alisema magari ambayo yametoka kiwandani yakiwa na taa hizo, hayatahusika.
“Hapa
nazungumzia taa za kuongeza. Lakini pia kuna magari kwa ajili ya
uwindaji huwa yanawekwa taa, lakini wanachotakiwa kufanya waweke kava,
wakati wote ziwe na kava,” alisema.
Alisema
wamiliki wa magari hayo ya kuwindia, wanatakiwa kuondoa kava hizo
wanapokuwa porini tu na kuongeza kuwa mtindo wa wamiliki wa magari
makubwa kuweka taa nyuma ya magari ambayo inamulika, matokeo yake mtu
anayemfuata anafikiri gari anakuja kumbe inakwenda mbele.
Post a Comment