Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
Zanzibar kuanzisha Duka Maalum litakalohusika na uuzaji wa mchele unaotokana na
Mpunga unaozalishwa na Wakulima pamoja na Taasisi za Zanzibar.
Amesema hatua hiyo muhimu itawapa
hamasa zaidi Wakulima wa zao hilo kuongeza juhudi za uzalishaji kupitia
Mradi wa kuongeza Tija na uzalishaji wa Mpunga Zanzibar ERPP
unaoonekana kuleta mafanikio makubwa ya kipato tokea kuanzishwa kwake
katika kipidi kifupi kilichopita.
Balozi Seif Ali Iddi ametoa agizo
hilo wakati akizindua rasmi uvunaji wa Mpunga wa Umwagiliaji maji kwa kutumia
Teknolojia ya Shadidi inayosimamiwa na Benki ya Dunia hapo katika bonde la
Mpunga Cheju Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Zanzibar inaweza kupunguza
uagizaji wa bidhaa za vyakula kama mchele kutoka nje ya nchi kutoka asilimia
80% hadi 40% ifikapo mwaka 2020 iwapo mkazo utaongezwa na wananchi walio wengi
Vijijini wanaojihusisha na Kilimo katika kutekeleza mradi huo.
Balozi Seif amewaagiza wataalamu
wote wa Sekta ya Kilimo Nchini kulazimika kutumia muda wao wa kazi kuwa karibu
zaidi na wakulima ili kufanikisha mradi huo na kuacha tabia ya kubakia Ofisini.
Ameeleza kwamba Kilimo cha mradi wa
shadidi ndio mkombozi pekeeunaoweza kuipunguzia Serikali kutumia fedha nyingi
za Kigeni kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara kuagiza bidhaa hiyo nje ya
Nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
amewashukuru washirika wa Maendeleo wa Kimataifa kwa jitihada zao za kuendelea
kuiunga Mkono Zanzibar katika kuimarisha Miradi ya Maendeleo.
Akisoma Risala kwa niaba ya
wakulima wa Mradi wa Kilimo cha Mpunga wa umwagiliaji Maji kwa kutumia
Teknolojia ya Shadidi Mmoja wa Wakulima hao alisema mradi huo
umeleta mafanikio makubwa yaliyopelekea Robo eka kuvuna kati ya Polo 13 na 14
ikilinganishwa na kilimo cha zamani walichoambulia Polo 8 hadi 9.
Mapema Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid Mohamed alisema Teknolojia hiyo ya Shadidi
ndio pekee inayoweza kuwakomboa Wakulima wakizingatia kufundishana kwa hatua ya
awali ya kuona.
Katika hatua nyengine Waziri huyo wa
Kilimo amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo tayari
imeshafanya mazungumzo ya pamoja na Muwekezaji Mzalendo watakaosimamia ufungaji
bora wa Bidhaa za Zanzibar kwa kutumia nembo maalum ili ziingie katika
soko la Kimataifa kiuhakika.
Post a Comment