0

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Manispaa ya Kigamboni kuhakikisha unasimamia ujenzi wa kisasa na kutenga maeneo maalumu ya wazi katika manispaa hiyo, ili kuepusha makosa ya ujenzi holela yaliyofanyika katika maeneo mengine jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa amesema manispaa hiyo mpya kwa sasa inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa majisafi na salama na wakazi wake wanatumia maji ya visima pekee ambayo si safi na salama.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri na Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam juzi katika ziara yake ya siku moja ya kujitambulisha na kukumbushana kuhusu uwajibikaji, Majaliwa alisema kwa sasa mji wa Dar es Salaam umejaa na eneo la Kigamboni ndio pekee la kukimbilia.

“Tunataka turekebishe makosa tukiyoyafanya katika mipango miji jijini Dar es Salaam, zingatieni matumizi bora ya ardhi, jengeni Manispaa ya Kigambo iwe ni mji wa kisasa, tengeni fukwe za jamii. Ikibidi hata muelekeze watu wajenge nyumba za aina gani,” alisisitiza.

Alisema kwa sasa mji wa Dar es Salaam umejengwa bila kuzingatia mipango miji kiasi cha kukosa maeneo nyeti kama bustani za kupumzikia wananchi pamoja na fukwe.

“Wenzetu wana hizi bustani za kumpumzikia watu wake zinasaidia hata kuchangamsha akili zao. Pale Dar es Salaam ufukwe wa jamii umebaki mmoja tu, Coco ambao kila mtu anakimbilia huko,” alisema.

Kwa upande wa Mgwandilwa, alisema manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha miaka hiyo wilaya hiyo inakuwa ni wilaya iliyojengwa kwa kuzingatia mipango miji na kuwa na miji ya kisasa.

Alisema kwa kuzingatia mipango miji hiyo, tayari halmashauri ya Kigamboni imetenga jumla ya viwanja 456 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ikiwa ni moja ya hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali za kuijenga Tanzania ya viwanda.

Akizungumzia changamoto za manispaa hiyo, Mgandilwa alisema pamoja na kwamba wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu, hali ya ukosefu wa majisafi na salama ni tishio na inahatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Alisema wilaya nzima ya Kigamboni inategemea maji ya visima ambapo hadi sasa vipo visima 83 vinavyomilikiwa na taasisi mbalimbali na jamii ambavyo navyo maji yake si safi na salama.

Aidha, alisema kwa upande wa sekta ya afya alisema pamoja na kwamba wilaya hiyo ina zahanati 17, kituo cha kimoja na hospitali kubwa moja, bado haijatimiza lengo la serikali linalotaka kila kata kuwa na zahanati moja.

Mkuu huyo alibainisha changamoto nyingine zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni uwepo wa mamlaka mbili zinazosimamia na kutawala eneo la ardhi ya Kigamboni hali inayosababisha mvutano na kuifanya wilaya hiyo ishindwe kuendelezwa kwa muda wa miaka nane sasa.

Alitaja mamlaka hizo kuwa ni Mamlaka ya Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA) inayotawala na kusimamia asilimia 12 na Manispaa ya Kigamboni inayosimamia na kutawala asilimia 88 ya ardhi ya wilaya hiyo ya Kigamboni.

Kuhusu ubovu wa barabara, Mgandilwa alisema kwa sasa wilaya hiyo ina barabara mbili tu kuu na zote ziko katika hali mbaya ambazoni ni barabara Kimbiji-Pembamnazi na Kibada- Mkuranga.

Waziri Majaliwa, akijibu hoja ya muingiliano wa mamlaka katika eneo la ardhi, alitaka mamlaka hizo zikutane na kujadili suala hilo ikiwa ni pamoja na kulitafutia ufumbuzi.

Post a Comment

 
Top