Wakati
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akidai kuwa hali ya
chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya, Serikali imesema
hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za wastani.
Zitto
alidai jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya
chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na
chakula cha kutosha miezi miwili.
Kwa
mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba
inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), imebaki
na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni cha kutosholeza siku
nane.
Hata
hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alijibu
madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha kutosha wala siyo cha
siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo
ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi
kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo
wakala haukununua chakula kingi.
“NFRA
inanunua chakula kwa kuangalia mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu
wakivuna sana maghala yao yanakuwa yamejaa na mahitaji ya chakula
yanakuwa madogo ndiyo maana Serikali hainunui chakula kingi. Miaka
miwili iliyopita Serikali ilinunua mahindi kwa wingi lakini yaliishia
kuharibika,” alisema Dk Tizeba.
Aliongeza
kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga ghala jingine lenye uwezo wa
kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa lenye uwezo wa tani
246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya 500,000.
“Kuna
maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko watavuna kama
kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi bila
vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo siwezi kutaja
kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila kinatosha siyo
kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” alisema Tizeba.
Juzi
wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani katika kata ya Kiwanja
cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema kauli ya Rais John
Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba Serikali haina shamba ni
kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa akiba ya chakula ya
kutosha.
Alidai
kuwa hali ya chakula nchini si nzuri, wananchi wanashuhudia namna bei
za vyakula zinavyopanda kila siku akidai kuwa bei ya sembe na mchele
zimekuwa juu na gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na uhaba
wa chakula kuwa mkubwa.
“Hali
ya chakula inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali
kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa
zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho
kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama
za chakula,” alisema Zitto.
Aliongeza
kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za chakula wakati kipindi kama
hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa na tani 459,561.
Takwimu
alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika ripoti ya BoT ya Novemba mwaka
jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016 hadi Julai 2016, akiba
ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi 49,632, lakini hadi Oktoba
mwaka huo iliongezeka hadi 90,476.
Ripoti
hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa chakula kwa mwaka jana na miaka
mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014 Januari, kulikuwa na tani
235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka 2015 Januari kukiwa na
tani 459,561 na Desemba 180,746.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven
Ruvuga alisema hali halisi kwa wakulima siyo nzuri kwa kuwa mvua
zilinyesha chini ya kiwango, hivyo kuna hofu ya ukosefu wa chakula cha
kutosha baadaye.
“Sasa
hivi nipo Kiteto na kwa kawaida mahindi yalipaswa kuwa tayari yameinuka
kufikia walau mabega ya mtu mzima, lakini nikiyatizama sasa bado yako
chini.
"Mwaka
huu kuna hatari ya ukosefu wa chakula na naishukuru Serikali kwa kuwa
imeanza kuchukua hatua katika maeneo yenye uhitaji,”alisema Ruvuga.
Aliongeza
kuwa Ghala la Taifa linapaswa kuwa na wastani wa tani 300,000 za akiba
lakini kama sasa zipo 90,476 zinaweza zisikidhi mahitaji ya kila mtu
hivyo ni vyema ikabuni mpango mbadala.
Post a Comment