0

Bilionea wakitanzania na mmiliki wa makampuni ya IPP Bwana Reginald Mengi aliwahi kusema kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa, “Mwogope mtu anayesema yupo na wewe ukigeuka nyuma hayupo. Huyo ni mnafiki.” Hayo ni maneno magumu lakini yana kitu kikubwa cha kujifunza ndani yake. Kuna jambo nataka tujifunze kwa kupitia ujumbe huo mfupi hasa wakati kama huu tunapoelekea kumaliza mwaka huu 2016 na kuutafuta mwaka 2017. Jambo hili ninalotaka ujifunze na kulizingatia ni juu ya “kufanya uchaguzi makini wa kuchagua marafiki au watu wa kushirikiana nao katika malengo na mipango yako uliojiwekea hadi hivi sasa kwa ajili ya mwaka ujao.”

Usikubali kutembea na kila mtu kwenye njia zako, bali amua kuweka uchaguzi sahihi wa kujua ni nani wa kwenda nae ili uweze kufanikisha malengo na ndoto yako uliyonayo. Kusema nitafanya jambo fulani na kila mtu, huku ni wazi si kila mtu ana uwezo wa kubebana na jambo unalotaka kufanya au kukupa nafasi ya kusogea mbele na kupiga hatua, yawezekana umeamua kuwa nae kwa sababu ya huruma, au uliwahi kusoma nae au ni rafiki yako wa zamani nk. Hapana. Hatuendi na kila mtu kanaani kwa sababu wote ni wa Israel ila ni wale walio na moyo wa utayari wa kwenda huko, na wale tu wenye nafasi ya kukubali magumu ya njiani kukubali kutembea pamoja nawe.
Wakati mwingine tumejikuta tunaingia katika maumivu makubwa kwa sababu ya kujaribu kuweka matumaini yetu kwa watu fulani pasipo kujua watu hao wanatuwazia nini ndani yao. Usiweke matumaini yako (expectations) kwa 100% kwa mtu ambaye hujampima na kumjua ana mwelekeo gani binafsi kwenye kuifata na kuishi ndoto yake mwenyewe na zaidi sana kwako wewe ambae umeamua kumshirikisha mambo yako uliyonayo. Usimtegemee mwanadamu kwa 100% bali amua kuweka uamuzi chanya wa kujisimamia wewe mwenyewe kama hatua za kwanza za kujijengea msingi mzuri wa kule unapoelekea, kisha kaa chini na utafakari kwa makini ni yupi unayeweza kwenda nae ili kuleta matokeo chanya kwenye maisha yako.

FANYA ZOEZI HILI:
1: Chukua kipande cha karatasi au notebook au diary yako ya mwaka 2017.
2: Orodhesha majina ya watu wa 5 au 10 unaotaka wakusaidie katika kutimiza malengo na ndoto yako kwa mwaka 2017.
3: Katika orodha ya majina yako amua kuchagua mtu mmoja au wawili tu utakaowashirikisha mara kwa mara kila kitu unachoendelea kufanya au unachofanya ili waweze kukuongoza na kukupa msaada juu ya unachofanya. Kumbuka amua kuwa na mtu mwaminifu na unayemwona anafaa kwa kile unacholenga wewe katika kukifanikisha. Usijaribu kuwa na kila mtu.
4: Watafute wahusika kwa kuwasiliana nao haraka. Usiogope. Jiamini.

KWA USHAURI ZAIDI:
Kwa ushauri zaidi ya namna ya kufikia malengo yako ya 2017 na hatimaye kuweza kutimiza ndoto yako uliyonayo, kuwa huru kuwasiliana nami kupitia mawasiliano yangu hapo chini ya website, nami nitakupa msaada wa bure kabisa. Usikubali kutembea mwenyewe bali kuwa karibu na mtu mwaminifu aliye na utayari wa kukusaidia na anayeweza kukuongoza (coaching) hasa katika kufikia ndoto yako.

JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Simu: 0767 500994 (WhatSapp Group – IshiNdotoYako)
Barua pepe: info@ishindotoyako.com
Ni Mimi mmiliki na mwanzilishi wa tovuti namba moja ya mafunzo ya kuhamasisha kwa lugha mama ya kiswahili, inayosomwa na watu wengi wanaotumia lugha hii ya kiswahili duniani. Nakupenda sana na usiache kutembelea mtandao huu mwaka ujao kwa kusudi la kujifunza zaidi na zaidi ili kupiga hatua ya kufikia ndoto yako. Nikutakie mwaka 2017 ulio na ushindi na mafanikio kiroho na kiuchumi zaidi.

Post a Comment

 
Top