0
Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi mh: dkt Ali Muhamed Shein amesema lengo la serikali ya mapinduzi Zanzibar kujenga skuli ya sekondari ya kwarara ni kuwaondolea usumbufu wanafunzi kwakuifuata elimu masafa ya mbali.



Rais Shein ameyasema hayo katika hafla fupi ya kuifungua skuli hiyo pamoja na kituo cha elimu ya habari ikiwa ni shamra shamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Dkt shein amesema kufunguliwa kwa skuli hiyo ni mkakati pia wa serikali ya mapinduzi Zanzibar  wa  kuwafikishia wananchi huduma muhimu karibu na makaazi yao ikiwemo huduma ya elimu.

Sambamba na hayo rais shein  amewataka wanafunzi kutohadaika na mambo ya kidunia na badala yake kusoma kwa bidii ili waweze kupata taaluma itakayowawezesha kujiajiri kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Nae waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar mh: Riziki Pembe Juma amewasisitiza wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuwaepusha na matatizo majiani yakiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia wakati wa kwenda na kurudi skuli.

Katika hatua nyengine katibu mkuu wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar bi Khadija Bakari Juma amewataka walimu na wanafunzi wanaoitumia skuli hiyo kuitunza ili iweze kutumia na kizazi kijacho.

Kilele cha sherehe za miaka 53 ya mapinduzi Zanzibar kitafikia hapo kesho katika viwanja vya amani stadium na zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.



Post a Comment

 
Top