WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Wajumbe wa Baraza la
Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kukutana na wamiliki wa taasisi za
kifedha kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo yenye gharama nafuu.
Akizungumza na wajumbe wa baraza hilo
nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es
Salaam, Mhe. Majaliwa amesema ni vyema wajumbe hao wakakutana na wamiliki wa
taasisi hizo za kifedha ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo yenye masharti
nafuu itakayowawezesha kukuza uchumi wao.
Amesema wananchi wanahitaji kuona ni namna gani Serikali
imejipanga kuwawezesha kiuchumi, hivyo baraza litoe muelekeo wa namna ya
wananchi watakavyoweza kufuga na kulima kitaalam ili waweze kupata tija.
Waziri Mkuu amesema asilimia 80 ya wananchi wanajishughulisha na
kilimo kama njia sahihi ya kuboresha uchumi. Pia ufugaji unaweza kusaidia jamii
ya wafugaji kupata tija, hivyo baraza liwasaidie kwa kuwapa mbinu sahihi za
kuboresha ufugaji wao.
Nae Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk. John Jingu amesema
wanaamini kuwa
uwezeshaji katika maeneo hayo utaleta matokeo ya haraka kwa wananchi wengi kwa
kuwa shughuli zao nyingi zimejikita katika maeneo hayo kinachotakiwa ni
kutafuta mbinu kutatua changamoto zilizopo ambazo ni ukosefu wa mitaji na
masoko ya uhakika kwa mazao.
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)
limezinduliwa Januari 8 mwaka huu na
kupanga kuanza kazi katika maeneo ya kipaumbele yatakayokuwa na tija kwa
wananchi ambayo ni kilimo, sanaa, ufugaji na uvuvi.
Post a Comment