Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameliomba Shirika
la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuisaidia Tanzania
kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini
ambao umepelekea mamia ya ekari za misitu kutoweka kutokana na ukataji wa miti
kwa ajili ya kutengeneza mkaa.
Ametoa
ombi hilo alipokuwa akifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa
Rais amesema pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na tatizo
la uharibifu wa mazingira ikiwemo mpango wa upandaji wa miti kote nchini lakini
bado msaada na nguvu zaidi inahitajika kutoka shirika hilo ili kuongeza kasi ya
kukabiliana na tatizo hilo nchini.
Makamu wa
Rais pia amehimiza wataalamu wa mazingira wajikite zaidi katika kutoa elimu kwa
wananchi watumie nishati mbadala kama gesi na makaa ya mawe ili kudhibiti
tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya
kutengeneza mkaa.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ERIC SOLHEIM
amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kukabiliana na uharibifu wa
mazingira na kusisitiza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali
Tanzania katika Uhifadhi wa mazingira nchini.
Nae, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba amesema
ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa UNEP hapa nchini ni fursa ya kipekee ya kufungua na
kuimarisha ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Tanzania na UNEP.
Makamba
amesema kuwa Serikali imetengeneza programu mpya Tano za mazingira ikiwemo
kupunguza matumizi ya mkaa ili kuhifadhi misitu,vyanzo vya maji,kushughulikia
taka na kujenga uwezo kama hatua mpya kabisa ya kukabiliana na uharibifu wa
mazingira nchini.
Post a Comment