WATU wawili, akiwemo mmiliki wa duka la dawa muhimu za binadamu katika
kijiji cha Itagata wilayani Manyoni, wanashikiliwa na Polisi mkoani
Singida kwa tuhuma za uzembe wa kusababisha kifo cha mjamzito, Heleni
Maduhu (29).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni mume wa marehemu, Bahame Kamuda (32) na Joseph
Hengwe (50) ambaye ni mmliki wa duka la dawa katika kitongoji cha
Kilulumo, kijiji cha Itagata Tarafa ya Itigi wilayani Manyoni.
Alisema tukio lilitokea kitongoji cha Lulanga kijijini hapo Januari 25,
mwaka huu saa 9.30 alasiri wakati mjamzito huyo akiwa njiani kupelekwa
Hospitali ya Misheni ya Itigi kwa matibabu zaidi kutokana na kuvuja damu
nyingi baada ya kujifungulia kwenye duka la Dawa la Hengwe.
Alisema kuwa siku moja kabla, mume wa mjamzito huyo alimpeleka mkewe
kwenye Zahanati ya kijiji Itagata ili kufanyiwa uchunguzi ambapo
inadaiwa muuguzi wa Zahanati hiyo, Grace Simon iliwaambia njia ya uzazi
ilikuwa haijafunguka; hivyo akawashauri warudi nyumbani.
Alisema kuwa aliporejea nyumbani hali ya mjamzito huyo ikawa mbaya hivyo
kumlazimu mumewe kumpeleka Zahanati ya jirani ya Misheni katika Kijiji
cha Mitundu kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, Kamanda Magiligimba alidai kuwa wakiwa njiani, mumewe aliona
hali ya mkewe inazidi kuwa mbaya zaidi, aliamua kumpeleka kwenye duka
la dawa muhimu linalomilikiwa na Hengwe lililopo jirani ambapo
alijifungua mtoto wa kiume.
“Kutokana na mjamzito huyo kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua,
mumewe aliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Misheni ya Itigi kwa
pikipiki lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufika mbali kabla ya mama
huyo kufariki dunia,” alisema Magiligimba.
IMEANDIKWA NA ABBY NKUNGU-HABARILEO SINGIDA
Post a Comment