Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo.
*****
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limevamia ofisi za
mtandao wa Jamii Forums (JF) na kufanya upekuzi na kuondoka na vifaa
zikiwamo kompyuta mpakato (laptop).
Askari hao walivamia ofisi hizo jana mchana wakiwa wamefuatana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo, wakafanya upekuzi na
kuwahoji baadhi ya wafanyakazi.
Baada ya kufanya upekuzi ndani ya ofisi hiyo walielekea nyumbani kwa
mkurugenzi huyo, kufanya upekuzi kabla ya kumrudisha rumande kwa vile
hakufikishwa mahakamani.
MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon
Sirro kwa simu ili kupata taarifa kwa kina, lakini haikuweza
kupokewa.
Juzi, akizungumza na MTANZANIA, mwanaharakati wa kutetea Uhuru wa
Mawasiliano, Simon Mkina, alisema Melo alikamatwa na kupelekwa Kituo
Kikuu cha Polisi ambako aliwekwa selo.
Alisema Melo anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia upelelezi wa makosa ya
mtandao kwa kushindwa kutoa taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wa
Jamii Forums ambazo polisi walizihitaji.
“Max (Melo)alifika kituoni hapo kuitika wito wa polisi wa Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, lakini alipofika Kituo Kikuu cha Polisi alinyimwa
dhamana kwa madai ya kuwapo amri kutoka kwa wakubwa,” alisema Mkina
akimkariri mmoja wa maofisa wa polisi.
Mkina alisema hata baada ya kuwasiliana na mwanasheria wa Melo, Nakazeel
Tenga na kushughulikia dhamana yake, ilishindikana kwa maelezo kuwa
alipaswa kulala kituoni hapo hadi jana.
Na HERIETH FAUSTINE-MTANZANIA DAR ES SALAAM
Post a Comment