Kabla hajajulikana na kuwa mtu maarufu kama hivi leo, mtu huyu
aliwahi kupambana na hali ngumu ya maisha ili kufikia mafanikio
aliyokuwa akiyatarajia daima. Namzungumzia si mwingine bali ni Walt Disney
ambaye ndani ya mwaka 1919 aliwahi kufanya kazi na mojawapo ya gazeti
la habari na kwa muda mfupi akafukuzwa kazi na bosi aliyemwajiri baada
ya kukosa maono na mawazo ya ubunifu katika kazi.
Mwezi Januari 1920, Disney kwa mara ya kwanza aliweza kuanzisha
kampuni yake ya muda mfupi inayojihusisha na masuala ya sanaa hasa
katika utengenezaji na uchoraji wa picha za katuni. Hata hivyo, pamoja
na kujituma katika kuanzisha kampuni yake ya kwanza, aliendelea na kazi
iliyokuwa ikimpatia fedha zingine za pembeni katika kampuni
iliyojulikana kwa jina la Kansas City Ad. Hakuishia hapo tu kwani baada
ya muda mfupi aliweza kuanzisha studio yenye mafanikio makubwa, lakini
haikuweza kuwa na faida ya kujitosheleza katika kuwalipa wafanyakazi
mshahara mzuri. Na katika muda mfupi kampuni yake iliingia katika madeni
hata kufikia hatua ya kushindwa kujiendesha na hatimaye kufilisika.
Lakini kushindwa haikuwa sababu kwake ya kutokujaribu tena, kwani
baada ya hapo Disney aliamua kuanzisha studio katika mji mkuu maarufu wa
kutengeneza filamu, Hollywood, California. Na kwa mara nyingine Disney
pamoja na mshirika wake Ub Iwerks kwa kupitia studio yake ya Walt
Disney, aliweza kutengeneza filamu ya kwanza ya katuni iliyoweza
kufanikiwa sana kibiashara na mauzo ijulikanayo kwa jina la Oswald the
Lucky Rabbit. Kwa kifupi huyu ndie mtu aliyekuja kufanikiwa sana hata
kufikia kushinda tunzo nyingi ndani ya jiji la Hollywood na kupata
mafanikio makubwa sana katika tasnia ya uzalishaji filamu, Disney ni
miongoni mwa watu waliokufa ingawa wanaishi kwa nguvu ya mawazo yao
yaliyokuwa na nguvu ndani yake na yanayoongea hadi leo.
Leo hii studio ya Walt Disney ni miongoni mwa studio maarufu sana
ndani ya jiji la Holywood, studio inayozalisha filamu nyingi kutoka
kwenye mji huo huku ikiwa si tu kwenye eneo la katuni kwa sasa bali hadi
filamu za kawaida. Kama umekuwa mfatiliaji wa karibu wa filamu kadhaa
zinazotengenezwa ndani ya jiji la Hollywood basi hautakosa kuona filamu
hata mojawapo yenye lebo ya Walt Disney kwa mwaka. Studio hii ndio
iliyomzalishia Disney utajiri mkubwa katika kipindi chake alichoishi
hadi hivi leo, na hata kufikia kumiliki maeneo makubwa katika nchi
nyingi duniani yenye majumba makubwa yajulikanayo kama Disneyland ili
kukutanisha watoto na wazazi wao kwa ajili ya michezo mbalimbali.
Jiulize ni mawazo au wazo gani ulilonalo ambalo linaweza kuwa sababu ya
kufanya ndoto yako kuwa halisi na kuleta mafanikio makubwa katika maisha
yako?
“All our dreams can come true if we have the courage to pursue them.” -Walt Disney
Haya ndio mambo matatu ya kujifunza kutoka kwa Walt Disney:
1: Haijalishi watu wanakuonaje, ukiamua kuamini uwezo ulionao utafanya mambo makubwa.
Mafanikio yako yapo njiani hata kama hauoni jambo hili kwa wakati
huu, kama ukiamua kuamini hadi mwisho uwe na uhakika utaona uhalisi
ukitokea. Haijalishi watu wanadharau uwezo mdogo ulionao kwa sasa ila
ukiamini unaweza na kuongeza bidii ya kufanya unachokipenda kila siku
pasipo kughairisha uwe na uhakika ipo siku utawashangaza watu wengi sana
waliokudharau na dunia itafahamu uwezo na mafanikio yako. Usikubali
kuwa miongoni mwa watu wale wanaosemwa kidogo tu kisha wanamua kukata
tamaa katika kuzifuata ndoto zao, amua kuchukulia kusemwa kama
changamoto ya kukupa nafasi ya kuendelea mbele zaidi.
Watu wengi wanapokutana na maneno ya watu huwa ni wepesi wa kukata
tamaa hata kuacha kutenda majukumu yao ya kila siku yanayowapelekea
kufanikiwa katika ndoto walizonazo. Jiulize kama Walt Disney angeamua
kukata tamaa na kusikiliza maneno ya bosi wake wa mwanzo kuwa hana
ubunifu hata kufikia kumfukuza kazi, je, leo hii tungepata kumjulia wapi
na kujifunza mambo haya mazuri kutoka kwake? Disney alifahamu uwezo
wake ndio maana pamoja na kusemwa hakukata tamaa bali alitumia maneno
yale aliyosemwa kama sehemu ya kumfanya kuongeza bidii (maneno yalimu-
encourage) baada ya kufukuzwa akatumia changamoto hiyo kutambua uwezo
mkubwa zaidi alionao hadi alipofanikiwa.
2: Usikubali kufeli mara moja kuwe kizuizi cha kuanza tena.
Mara nyingi huwa tunatamani tupate mafanikio ya haraka yasiyopitia
changamoto yoyote ile, na hata pale inapotokea kushindwa katika jambo
fulani tunajikuta tunakata tamaa kwa haraka, pasipo kufahamu kuwa hakuna
mafanikio yoyote yanayoweza kutokea kwenye maisha yetu pasipo kupitia
changamoto nyingi zinazoweza kutuimarisha na kutufanya kuwa imara hapo
badae. Kumbuka kila unapojikwaa na kuanguka mahali fulani hiyo ni njia
mojawapo ya kukusaidia kupata mbinu na mikakati mipya itakayokufanya
uimarike katika kitu unachokifanya.
Maisha yako ya mafanikio yanategemea sana unavyokubaliana na
changamoto unazokutana nazo kila siku na kuchukua hatua ya kuzitafutia
majibu ili kukuzalia mawazo mapya ya kukupeleka mbele zaidi. Jiulize
ulipofeli kwenye jambo ulilokuwa umeanza kulifanya, je, ulikata tamaa
kufanya tena au uliamua kurudisha moyo wako nyuma na kurejea kufanya kwa
mara nyingine ili kuleta matokeo?
3: Chunguza katika mawazo mengi uliyonayo, amini lipo wazo moja la kukutoa.
Si watu wengi wenye tabia ya kuandika mawazo wanayoyapata kila siku
na kuyafatilia kama njia yao ya kutokea na kufanikiwa. Jiulize ni mawazo
gani niliyonayo ambayo naweza kuyageuza kuwa fedha na kuleta utajiri
mkubwa katika maisha yangu? Chunguza mawazo yako mengi uliyonayo kisha
amua kuchagua wazo moja unaloona katika hilo unaweza kulisimamia kwa
kutoa nguvu na muda wako mwingi kila siku (focus- concentration) ili
kuleta matokeo chanya kwenye maisha yako. Usiruhusu mawazo yako
uliyonayo muda huu kupita pasipo kuyachunguza na kuyachukulia hatua za
kivitendo ili kuzaa mafanikio halisi katika maisha yako.
Leo hii amua kuanza kuorodhesha mawazo yote uliyonayo katika kitabu
chako (ideas book), kisha chagua wazo moja unaloona kwa kupitia hilo
unaweza kulitekeleza kwa haraka kulingana na mazingira uliyonayo kwa
sasa. Fanya utafiti kama hatua ya awali inayoweza kukusaidia kufahamu
kama wazo lako linaweza kutekelezeka (applicable) kwenye mazingira
uliyonayo, huku ukiweka nguvu kubwa ya kufahamu soko la kitu unachotaka
kufanya. Usijaribu kuanza kufanya biashara au jambo lolote lile pasipo
kufahamu soko la bidhaa au huduma unayotaka kutoa. Chunguza soko la wazo
ulilonalo kisha amua kuwekeza nguvu na muda katika utekelezaji baada ya
kufahamu nguvu ya wazo lako ndani ya soko.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
“Money doesn’t excite me my ideas excite me.” -Walt Disney
JAMANI NAOMBENI MSAADA WA HIZO KATUNI ZINAVOCHORWA KAMA NI KWENYE COMPUTER AU KARATASI
ReplyDelete