Kuna watu fulani wanaweza kuja kwenye akili yako haraka hasa pale
unapofikiri kuhusu mafanikio. Watu kama vile Steve Jobs, Elon Musk,
Larry Page, Bill Gates, Mohamed Dewji. Ni ukweli usiopingika kuwa kila
mtu anatamani sana kufikia uhuru wa kifedha na kuwa na mafanikio makubwa
kama watu wengine wowote walivyofanikiwa leo. Umewahi kujiuliza ni nini
walichokifanya watu hao waliofanikiwa hadi kufikia mafanikio unayoyaona
kwao katika siku ya leo, na nini wanachokifanya kila siku ikiwa kama
wajibu unaowaweka katika muonekano tunaouona kwao kila siku.
Wakati mwingine tunaweza kutamani kuwa kama watu fulani katika maisha
yetu pasipo kutambua kuna wajibu na mambo tunayotakiwa kuwajibika ili
tuweze kufikia hatua ya mafanikio tunayoyataka. Kumbuka hakuna mtu
aliyeweza kufanikiwa moja kwa moja pasipo kupitia changamoto na
kukataliwa mara nyingi, ila tumekuwa ni watu wenye tamaa ya kutafuta
mafanikio kama watu fulani pasipo kuangalia gharama za mahali
walikopitia watu hao. Huwezi kufanikiwa nje ya changamoto za kila siku
unazokutana nazo, hii ni kukusaidia kukupa misuli ya mafanikio ya kule
unakoelekea.
Hapa chini kuna mambo madogo niliyokuandalia ambayo watu
waliofanikiwa wanafanya kila siku, hii ni baada ya kuchuguza kwa kina
watu waliofanikiwa wanatabia gani zinazowaletea mafanikio na kuendelea
kufanikiwa kila leo.
1: Wanaweka mwelekeo kwenye mambo machache yenye tija, zaidi ya kuwa bize pasipo sababu.
Kulingana na Tim Ferris, mwandishi wa kitabu cha The 4-Hour Workweek anasema kuwa, “Kufanya
vitu vingi hakusaidii kuleta matokeo unayoyataka. kuwa bize pasipo
jambo la msingi ni sehemu mojawapo ya kupoteza muda mwingi na matokeo
yake ni kutokufanikiwa kabisa au kufanikiwa kwa kiwango kidogo sana.” Sijafahamu
ni mara ngapi unakuwa bize kiasi cha kushindwa hata kula, je, umekuwa
bize kwa faida au kwa hasara? Ni mara ngapi umeangalia jambo
unalolifanya kama lina matokeo makubwa kwenye ndoto yako uliyonayo? Watu
wengi waliofanikiwa wanachukua muda wao mwingi kufanya mambo yenye
kuzalisha faida kila siku katika ndoto zao, wakati watu wengi
wasiofanikiwa wanapigana kuwa bize na kujichosha kwa mambo mengi yasiyo
na tija na mwelekeo chanya katika ndoto walizonazo. Jiulize kila
unapotaka kufanya jambo fulani kila siku, Je, lina matokeo gani katika
ndoto yako uliyonayo? Kwepa kuwa bize pasipo sababu za msingi kwenye
maisha yako.
2: Wanaamka mapema kila siku.
Wakati nasoma kitabu cha Think like billionaire cha Donald
Trump ambaye ni bilionea na mfanyabiashara wa majumba na majengo makubwa
nchini Marekani, na ambaye kwa sasa ni Rais mteule wa taifa hilo kubwa
duniani alinishangaza baada ya kuona muda wake wa kila siku wa kulala na
kuamka anasema, “Don’t sleep any more than you have to. I usually
sleep about four hours per night. I’m in bed by 1 A.M and up to read the
newspapers at 5 A.M. That’s all I need, and it gives me a competitive
edge.” Kama bilionea na Rais wa Marekani anaweza kulala masaa manne
kila siku, saa 7 usiku ndio anaingia kitandani kulala kisha saa 11
alfajiri amekwisha amka na kuanza kujisomea, jiulize wewe huwa unalala
na kuamka muda gani kila siku?
Hii si tabia ya Donald Trump tu bali tabia hii utaikuta kwa watu
wengi waliofanikiwa katika dunia kama Barack Obama, Aliko Dangote,
Mohamed Dewji, Bill gates na wengineo. Sergio Marchionne ambaye ni
mmiliki wa Fiat Chrysler Automobiles na Ferrari, tajiri huyu huwa
anaamka muda wa saa 9:30 usiku na kufatilia hali ya mwelekeo wa soko la
fedha la Ulaya kila siku. Tim Cook ambaye ni mmiliki na mwendelezi wa
kampuni ya Apple kwa sasa baada ya Steve Jobs, baada ya kufatilia maisha
yake kwa karibu nikakuta ni mtu anayeamka na kuanza siku yake kila siku
muda wa saa 4:30 alfajiri kwa ajili ya kutuma barua pepe kwa
wafanyakazi na washirika wa kampuni yake. Jeffrey Immelt, huyu ni
mmiliki na mwendelezi wa kampuni ya General Electric anayeamka kila siku
muda wa saa 11:30 alfajiri kwa ajili ya kutimiza majukumu yake ya siku
husika. Jiulize kama watu hawa wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa namna
hiyo, nini kinachowafanya na kuwasukuma kuamka muda huo? Je, wewe
umefikia wapi kwenye ndoto yako, huwa unaamka muda gani kila siku?
3: Wanaweka mwelekeo (focus) kwenye kutengeneza timu bora ya ushindi.
Kocha maarufu na tajiri Phil Jackson katika mchezo wa “basketball” nchini Marekani aliwahi kusema, “The strength of the team is each individual member. The strength of each member is the team.”
akimaanisha kuwa uwezo wa timu upo kwa kila mtu mmoja mmoja ndani ya
timu. Na uwezo wa kila mtu mmoja upo kwenye timu yenyewe. Hii inaonyesha
ni jinsi gani watu waliofanikiwa wanavyofahamu na kutilia maanani watu
wanaoweza kuwasaidia kutimiza ndoto zao. Huwezi kutimiza ndoto zako wewe
binafsi bali unahitaji watu wa kukusaidia kufanya hivyo. Usijaribu
kufanya jambo peke yako katika maisha, jaribu kuamua kushirikisha watu
wanaoweza kukubeba ili kukufikisha katika hatima ya ndoto yako. Ushindi
unatokea pale penye ushirikiano bali mafarakano hupoteza mwelekeo wa
kufanikiwa haraka.
“Coming together is a beginning. Keeping together is progress. Working together is success.”
-Henry Ford
4: Wanaweka mwelekeo kwenye kufanya mambo madogo yenye tija ili kusogea mbele.
Kuna dhana mojawapo inayosema kwamba, huwezi kumaliza tembo mmoja kwa
mara moja. Unahitaji kumgawa vipande vidogo vidogo hadi utapommaliza.
Henry Ford anasema pia, “Nothing is particularly hard if you divide it into small pieces.”
Hakuna kitu kinachoweza kuwa kigumu kama utaamua kukigawanya kwenye
vipande vidogo vidogo. Wapo watu wanatamani kutimiza ndoto kubwa
walizonazo kwa wakati mmoja na pale wanaposhindwa kufanya hivyo
wanajikuta wanakata tamaa mapema, hii ni mbaya unahitaji kufahamu
umeumbwa kufanya kulingana na uwezo wa ufahamu na nguvu ulizonazo.
Huwezi kufanikisha kila kitu kwa wakati mmoja, ila unapoamua kugawanya
lengo lako kubwa kwenye vipande vidogo vidogo unakuwa unajisaidia
binafsi kuweka mwelekeo (focus), na hapo itakusaidia kumaliza haraka
kitu kikubwa ulichokuwa hutegemei kukimaliza mapema.
5: Watu waliofanikiwa ni watu wa kutafakari (meditation).
Kulingana na Oprah Winfrey juu ya eneo la kutafakari anasema, “Kutafakari
kumeleta matokeo mazuri, makubwa na yasiyoelezeka katika maisha yangu.
Usingizi mzuri. Kuboresha mahusiano yangu na familia yangu na hata
wafanyakazi wangu. Kuongeza ufanisi na ubunifu katika kazi
zilizonizunguka.” Watu waliofanikiwa huwa ni watu wenye kutoa muda
wa kutafakari kwenye mambo muhimu yanayowasukuma kwenye hatima ya ndoto
zao. Mwanzilishi wa Def Jam Record, Russell Simmons anasema, “Kutafakari ndio kumefanya maisha yangu kugeuka moja kwa moja hadi kufikia hapa nilipo”. Jiulize ni mara ngapi umekuwa ukitoa muda wa kutafakari juu ya maisha yako na kule unapoelekea?
Unapotoa muda mwingi wa kutafakari juu ya maisha yako hasa dhidi ya
kile unachokitaka ni rahisi sana kuzaa mawazo (ideas) mengi ya
kukusaidia kuchukua hatua za haraka na kukupa mwanga wa mafanikio yako
unayoendea. Jifunze kutoa dakika 15 hadi 30 au lisaa limoja kila siku
kwa ajili ya kutafakari juu ya kule unapotaka kwenda na namna ya
kuchukua hatua madhubuti za kufika katika kilele cha mafanikio yako.
6. Ni waangalifu juu ya miili yao.
Mazoezi ya mara kwa mara hayatoshi peke yake kukufanya kuwa kwenye
hali nzuri ya kiafya, lakini akili iliyojaa kujiamini na kujengwa kwenye
misingi ya kulishwa kitu kipya kila siku ni muhimu pia. Mmiliki wa
kampuni ya Metl Group nchini Tanzania, Mohamed Dewji, yeye anatumia
lisaa limoja kila siku jioni kwa ajili ya mazoezi ya mwili wake. Mmiliki
wa Starwood Hotels & Resorts, Frits van Paasschen, anafanya mazoezi
ya kukimbia maili 10 kila siku kuanzia muda wa asubuhi saa 12. Rais wa
Marekani Barack Obama anakimbia maili 3 au mara nyingine anatoa dakika
45 za kufanya mazoezi kwa siku, ndani ya siku sita kwa wiki. Mazoezi
yanaifanya akili ya mtu kuchangamka na kuiweka katika afya kwa kufikiri
haraka zaidi kuliko mtu hasiyefanya hivyo.
7. Wanaweka Usawa katika mambo yao wanayofanya.
Kufanikiwa katika mambo yako mengi mazuri unayotaka, unahitaji kuweka
usawa (balance) na kuwa mwangalifu zaidi juu yako binafsi. Watu
waliofanikiwa ni waangalifu zaidi katika kuweka usawa juu ya maeneo
mbali mbali ya maisha kama vile kutengeneza kipato chao, kutoa muda wa
kupumzika na familia zao au watu wanaowapenda, kutoa muda wa ibada, na
hata kufanikisha malengo yao binafsi waliyonayo. Ni vizuri kuelewa
umuhimu wa kila jambo zuri unalopaswa kulitimiza katika maisha yako na
kuweka usawa juu yake katika kulitekeleza kwa kila moja. Kila jambo lina
umuhimu wake katika maisha, ibada ina umuhimu wake na biashara ina
umuhimu wake pia; huwezi kusema unatafuta pesa tu hata kusahau ibada
katika maisha yako. Ni vizuri kujifunza kuweka usawa juu ya kila jambo
ili uweze kufanikiwa na kubaki katika mstari mzuri wa kuendelea
kufanikiwa na kusaidia wengine kupitia maisha na mafanikio yako.
8. Wana mwelekeo chanya muda mwingi.
Katika kitabu chake cha The Happiness Advantage, Shawn Achor
anaelezea utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa, dokta yoyote
anayemwandaa mgonjwa wake kifikra (hali chanya) kabla ya kumpima au
kuchunguza ugonjwa anaoumwa ndani yake, anamweka mgonjwa katika hali ya
nzuri ya kujiamini hata kama mgonjwa huyo alikuwa hawezi kabisa. Na kwa
sababu hiyo inamsaidia yeye kufanya uchunguzi wa kutosha na ulio sahihi
kwa karibu 20% anazookoa. Watu wengi waliofanikiwa siku zote wana
matumaini na mawazo chanya dhidi ya ndoto walizonazo, hawakati tamaa
mapema bali wanatanguliza ushindi mbele yao hata kama wanapitia katika
hali ngumu. Ni watu wenye kutanguliza hali chanya kwenye kila jambo ili
kuharakisha mafanikio yao.
“Optimism
is the most important human trait, because it allows us to evolve our
ideas, to improve our situation, and to hope for a better tomorrow.”
-Seth Godin
9. Wanaendeleza vitu vizuri walivyonavyo na si watu wa kukata tamaa mapema.
Leo hii tunawaona watu kama Serena Williams, Oprah Winfrey, na J.K
Rowling wanaendeleza vipaji na vitu wanavyopenda kuvifanya. Watu hawa
wapo tayari kuendelea kufanya wanachokipenda kwa kuwa wanajua siri ya
kufanikiwa ipo kwenye kufanya kile unachokipenda pasipo kuchoka. Ni watu
wenye kuweka malengo na kuchukua hatua za haraka kuyafanikisha,
wanajifunza kutokana na makosa. Siku zote ni watu wenye ramani ya mahali
kule wanapoelekea na wakati mwingine wanatumia “notebook” zao
kuchora maisha yao ya badae ya kule wanapotaka kufika. Huna haja ya
kukata tamaa bali jifunze kwa waliokutangulia na kufanikiwa mbele yako
huku ukiamini “ipo siku yako” nawe utafanikiwa.
10. Wanatengeneza njia ya mafanikio yao.
Watu wanaofanikiwa ni wale wenye kujua wajibu wao dhidi ya mafanikio
wanayoyahitaji, kwa kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya au
kama ajali. Kila mtu aliyefanikiwa leo alijua anayo haki ya kufanikiwa
kama wengine waliotangulia mbele yake. Katika kitabu cha Think and Grow Rich cha Napoleon Hill anasema, “You are the master of your destiny.” akimaanisha
kuwa wewe ni kiongozi au mwamuzi wa hatima yako. Wewe ndio
unayechochea, unayeongoza, unayeendesha mazingira yako yote ya
mafanikio. Wewe ndiye unayeweza kuyaweka maisha yako kwa jinsi yoyote
vile unavyotaka. Amua leo kuongoza maisha yako kwenda katika mafanikio
makubwa unayoyahitaji hasa ya kufikia kilele cha ndoto yako.
11. Wana marafiki waliofanikiwa.
Mwalimu wa mafanikio Jim Rohn aliwahi kusema, “you are the average of your five closest friends.” Unakuwa
vile unavyokuwa kutokana na marafiki zako watano ulio na ukaribu nao.
Watu waliofanikiwa wanafahamu hili, ndio maana muda mwingi wanatumia
kutafuta ukaribu na washauri wazuri (mentor) na watu wengine
waliofanikiwa. Huwezi kufanikiwa kwa kiwango cha juu nje ya watu ulionao
karibu kila wakati. Jiulize na kutathmini marafiki ulionao kama
wanachagia kwa kiasi kikubwa mafanikio kwenye ndoto yako uliyonayo?
12. Wanahamasisha watu wengine kufanikiwa kama wao.
Steve Jobs mmiliki aliyepita wa kampuni ya Apple kabla hajafariki,
alikuwa akitoa muda mwingi katika maisha yake kusaidia watu wengine
katika kuwafanya kuwa wabunifu. Kulingana na Steve Jobs mwenyewe aliwahi
kusema, “ubunifu ni njia mojawapo ya kuunganisha vitu na watu.” Unapochukua
muda kuwauliza watu wabunifu wamewezaje kufanya kitu fulani, wanajiona
hawakustahili kwa sababu ukweli ni kwamba sio wao tu waliofanya hivyo,
lakini waliona picha hiyo ndani yao tangu muda. Ndipo walipoamua
kuunganisha picha hiyo hatua kwa hatua, siku hasi siku hadi ilipokuwa
halisi kwenye mazingira ya nje. Jiulize ni muda gani unatoa kila siku
kusaidia wengine kufikia ndoto zao walizonazo ndani yao?
Mohamed Dewji anasema, “When God blesses you financially, don’t raise your standard of living, raise your standard of giving.”
Akimaanisha kuwa Mungu anapoamua kukubariki kifedha, hutakiwi
kuendeleza maisha yako pekee, bali ni wakati pia wa kutoa kwa wengine.
Watu waliofanikiwa wanajua namna ya kutoa na kuhamasisha watu wengine
kufikia katika mafanikio wanayohitaji.
13. Wana ratiba thabiti kwa ajili ya majukumu yao ya kila siku.
Rameet Chawla, mwanzilishi wa Fueled,
anaamini kuwa na ratiba thabiti inamsaidia mtu kuwa na mwelekeo mzuri
katika kutimiza majukumu yake muhimu ya siku. Unapoamua kutengeneza
ratiba yako kila siku unakuwa unaokoa muda mwingi wakati wa utakelezaji.
Ni muhimu kama unahitaji kuona unafanikiwa kwenye malengo yako jifunze
kuwa na ratiba maalum inayoweza kukuongoza ili uweze kufanikiwa mapema
zaidi. Usiwe kama mtu anayetoka ndani ya nyumba yake na kupanda daladala
pasipo kufahamu ni wapi anapokwenda. Weka ratiba kisha amua kuifuata
ikiwa kama ramani ya kukupeleka kwenye kilele cha mafanikio yako.
14. Watu waliofanikiwa wana mipango ya kina ya kutekeleza.
Kabla ya kuondoka ofisini kwake muda wa usiku, Kenneth Chenault,
ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa American Express, huwa anaamua
kuandika mambo makuu matatu ya anayotaka kuyatekeleza katika siku yake
inayofuata, kisha anatumia orodha ya mambo hayo kuanza siku yake mpya.
Ni ngumu sana kwa mtu kufanikiwa katika ndoto yake kama hataona umuhimu
katika malengo na vipaumbele vyake alivyonavyo. Watu waliofanikiwa
wanapangilia mambo yao kabla ya kuanza siku inayofuata, huku watu
wengine hawatoi umuhimu wa kufanya hivyo na hii ndio sababu na kikwazo
kikubwa kwa watu wengi kufanikiwa na kufikia kusudi na ndoto za maisha
yao.
Leo hii amua kutokuanza siku yako mpya kabla ya kuandaa malengo na
kuweka vipaumbele vyako vya kutimiza kila siku. Andaa vipaumbele vyako
vya muhimu usiku kabla hujaanza siku mpya, au amua kuandaa pale
unapoamka alfajiri na mapema. Angalia ni mambo gani ya muhimu ya
kutekeleza katika siku husika, kisha amua kuwekeza nguvu zako zote ili
kuleta matokeo chanya na makubwa kwenye maisha yako. Alex MacKenzie
aliandika, “Action without planning is the cause of every failure.” akiwa na maana kuwa, kuchukua hatua pasipo kuwa na mipango ni sababu inayopelekea watu wengi kufeli kila wakati.
15. Watu waliofanikiwa kamwe si watu wa kughairisha mambo yao.
Mwanamama ambaye ni Mwandishi wa vitabu Karen Lamb aliwahi kuandika, “Mwaka mmoja kutokea sasa utajutia kutokufanya kile unachoona haupaswi kufanya leo.”
Watu wengi wanapenda kutoa sababu za kutokuchukua hatua dhidi ya mambo
wanayotakiwa kutekeleza, hii ndio sababu iliyowafanya watu wa aina hii
kushindwa kufanikiwa kwa haraka. Wakati nafatilia watu wengi
waliofanikiwa nikakuta ni tofauti sana na watu wengi ambao
hawajafanikiwa, watu waliofanikiwa wanapenda kutekeleza mipango yao kwa
haraka pasipo kujiuliza maswali mara mbili mbili, na hii ndio sababu ya
wao kuendelea kufanikiwa kila kukicha. Jiulize ni kitu gani
ulichokipanga kwa muda mrefu ambacho umekuwa ukikitolea sababu ya
kutokuchukua hatua?
Post a Comment