Siku moja nilibahatika kumsikiliza mwalimu wa masuala ya mafanikio
Darren Hardy ikizungumzia hadithi moja iliyonihamasisha zaidi katika
kufuata na kutimiza malengo yangu. Hadithi hii ya kuhamasisha zaidi
ilimuhusu mmiliki mmoja wa biashara aliyekuwa amepata hasara katika
biashara yake, iliyomfanya aingie katika wasiwasi mkubwa kutokana na
kutokufahamu hakika ni wapi pakupata tena fedha kwa ajili ya kusimamisha
na kuifanya biashara yake kuendelea kusimama.
Katika kipindi hicho cha kujihoji na kutafuta jibu ni wapi pakupata
fedha, ghafla alikuja mwanaume mzee sana na kukaaa karibu na mahali
alipokuwa amekaa. Mzee yule akamuuliza, kwa nini una wasiwasi mkubwa
mwanangu? Mfanyabiashara yule akamjibu yule mzee kwa kumwambia kuhusu
uhitaji wake wa haraka wa kuhusu fedha za kuendeshea biashara yake
iliyopata hasara kubwa na kutaka kufa. Ndipo yule mzee akasema, ninaweza
kukusaidia kwa kukupatia cheki ya hela, kisha tukutane siku kama ya leo
mwakani mahali hapa kwa ajili ya kunilipa. Kisha yule mzee hakukawia
akaondoka muda ule ule mahali pale.
Baada ya yule mzee kuondoka, ndipo mfanyabiashara yule alipoamua
kufungua cheki aliyopewa na kuamua kusoma ndani na ndipo akakuta kiasi
cha $500,000 zilizosainiwa chini kwa jina la John D. Rockefeller. Ndio.
hakuamini, alikuwa ni John D. Rockefeller aliyekuwa tajiri mkubwa sana
duniani wa kipindi hicho ambapo kwa leo hii tunaweza kumpa hadhi ya mtu
kama Bill Gates. Kwa mshtuko na furaha kubwa aliyoipata mfanyabiashara
yule, hakuamini kabisa kama tatizo la fedha alililokuwa nalo limeondoka
kwa ghafla namna ile. Jambo hilo lilimfanya kupata matumaini makubwa na
kuwa mtu mwenye shauku kubwa ya kuendelea kufanya biashara yake kwa upya
kabisa.
“It takes no more time to see the good side of life than to see the bad.”
-Jimmy Buffett
Aliamua kuchukua cheki ile kisha akaiweka mahali salama pasipo
kuibadili katika fedha taslimu bali alihifadhi kama ilivyo hadi yule
mzee atakaporudi. Baada ya hapo akajikita zaidi katika biashara yake na
kufanya kazi kwa nguvu zote kwa kutumia njia mbadala. Alikuwa tayari
kufanya biashara na kuongeza faida zaidi kwa kujikita kwenye mikakati
mipya ya kumfanya atengeneze faida zaidi ili kuzuia hasara kundelea
kudidimiza biashara yake anayoifanya. Alibaki akishikilia cheki yenye
nusu ya milioni dola aliyokuwa amehifadhi pasipo kuitumia wala kuigusa
kwa kitu chochote kile.
Baada ya muda kwenda na mwaka mmoja kupita, mfanyabishara yule
aliamua kurudi mahali pale alipokutana mara ya kwanza na John D.
Rockefeller akiwa na cheki yake mkononi. Mzee yule alijitokeza kwa mbali
akija kwa mara nyingine hadi mahali pale alipokaa mfanyabiashara yule.
Ndipo mfanyabiashara yule alipoamua kumshawishi mzee yule kupokea cheki
yake aliyompatia na kurudisha shukrani zake kupitia msaada wake, lakini
ghafla muuguzi mmoja alikuja akikimbia huku akijaribu kumzuia yule
mfanyabiashara kutokufanya chochote. Muuguzi yule alisema, mtu huyu
(yule mzee) amejaribu kuondoka nyumbani mara kwa mara na kuanza
kuzunguka kwa watu na kujaribu kuwashawishi watu kuwa yeye ni John D.
Rockefeller.
Muuguzi yule aliamua kuanza kumwomba msamaha mfanyabiashara yule
dhidi ya kitendo alichokifanya mzee yule juu yake. Ndipo mfanyabiashara
yule akashikwa na hali ya juu ya mshangao na kupigwa butwaa dhidi ya
kile anachokisikia muda ule akijiuliza maswali kwamba, mwaka mzima
amekuwa ni mtu wa kufanya kazi kwa bidii na kwa kujitoa kwa kufanya
mikakati mingi ya kunusuru biashara yake kuanguka moja kwa moja, na hata
kufikia kuanza kutengeneza faida tena, lakini akifanya hivyo kutokana
na ushawishi mkubwa aliokuwa anaujenga katika akili yake kwa ajili ya
kunusuru na kuweka salama nusu ya mamilioni ya dola alizokabidhiwa ili
kujenga uaminifu. Lakini ghafla anakuja kutambua kuwa zile fedha
hazikuwa za kweli ingawa zilimfanya kuamsha ari mpya (morale) ya kufanya
kazi kwa bidii na hata kufikia kurudisha biashara yake katika mazingira
mazuri. Hii ilimpa nafasi ya kujenga ujasiri mpya ndani yake ulioweza
kumsadia kufanikisha mambo mengi katika maeneo mengine ya maisha yake.
Kuna mambo 3 tunayojifunza katika habari hii uliyoisoma na wewe mahali hapa:
1: Jiulize. Unahitaji nini cha kukuhamasisha ili kuchukua hatua dhidi ya hatima ya kile ulichokata tamaa kukifanya.
Mara nyigi huwa tunapitia katika nyakati ngumu na zenye changamoto
nyingi katika maisha yetu. Jiulize ni hatua gani unayochukua kukunusuru
na kukata tamaa pale unapopitia katika wakati mgumu ili kukuhamasisha
usikwame na kuacha kuchukua hatua dhidi ya kutimiza ndoto zako. Hakuna
mtu ambaye hapitii au hajawahi kupitia changamoto katika maisha yake,
ila utofauti uliopo kati yetu ni namna gani tunavyoweza kushikamana na
changamoto hizo ili kunusuru maisha yetu yasitoke nje ya mfumo mzima wa
mambo yetu tunayofanya kila siku yanayotupelekea katika kufikia katika
mafanikio yetu tunayoyataka.
Kila unapopitia changamoto fulani ni rahisi sana kujilaumu na kulaumu
watu wengine dhidi ya hali yako nzima unayopitia katika maisha, lakini
ukweli ni kwamba ni mara ngapi wewe binafsi umekuwa ukiwajibika dhidi ya
maisha yako ili kufikia hatua ya kujipa nguvu dhidi ya safari yako ya
kufuata mafanikio ya ndoto yako. Hakuna mtu wa kukupa kila kitu
unachotaka au unachozani kinaweza kuwa msaada mkubwa kwako wa
kukufanikisha moja kwa moja katika ndoto uliyonayo. Unapaswa kufahamu
wewe ndiye dreva wa maisha yako unayetakiwa kuendesha gari lako kwa
makini zaidi hata kama utapita kwenye milima na mabonde mengi, kikubwa
ni kutazama wapi unakoelekea ili uweze kufika salama na kwa wakati
sahihi.
2: Una uwezo mkubwa ndani yako. Tafuta mtu wa kukuhamasisha na kukuongoza ili kukutia nguvu zaidi kuchukua hatua.
Mfanyabiashara tuliyemsoma hapo juu kwenye stori yake, tunaona
hakuweza kufanya lolote baada ya kushindwa kujua ni wapi pakupata fedha
zitakazomsaidia kuendelea kuinua na kusimamisha biashara yake mpya.
Lakini baada ya kukutana na mtu aliyempatia cheki bandia ingawa wakati
huo hakujua kama amepokea cheki bandia, alijikuta ghafla akipata nguvu
ya kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kutunza uaminifu kwa tajiri mkubwa
aliyempatia fedha zile hata pasipo kuzitumia fedha alizopokea. Hii
inaonyesha ni jinsi gani alivyokuwa na shauku ya kuonyesha uaminifu wa
kiwango cha juu sana hasa kwa mtu mkubwa kama yule ambaye kwa uhalisia
alijua fika ni John D. Rockefeller kabla ya kuzibitika si kweli.
“I’m a success today because I had a friend who believed in me and I didn’t have the heart to let him down.” -Abraham Lincoln
Ukweli ni kwamba ili mtu yoyote afanikiwe anahitaji watu wanaoweza
kumpa hamasa kila siku hasa katika eneo lake la “field” analofanya. Hii
inamsaidia mtu kuwa mwenye nguvu na hata kuamsha ari (morale) ndani ya
mtu ya kufanya kazi kwa bidii pasipo kukata tamaa dhidi ya changamoto
anazokutana nazo kila mara. Nipo hapa kukutia moyo kuwa amini unaweza
kufanya lolote lile unaloona kwako ni gumu hadi hivi sasa, jiamini na
amni unaweza, ishi ndoto yako.
3: Ili ufanikiwe katika eneo lolote lile maishani unahitaji kiwango cha juu sana cha ujasiri ndani yako.
Kuna msemo mmoja wa kiswahili unaosema uoga wako ndio umasikini wako.
Tunachokiona kwa huyu mfanyabiashara ni ujasiri wa ajabu na nidhamu ya
hali ya juu ya kuweza kukaa na cheki yenye kiasi kikubwa cha fedha
pasipo kuchukua uamuzi wowote wa kwenda benki hata siku moja kwa ajili
ya kuzitoa. Kama ningekuwa ni mimi, naamini yawezekana ningekuwa tayari
nimeenda benki haraka sana kwa ajili ya kutoa fedha zile, kwa sababu
tayari nilikuwa kwenye kiwango cha juu cha kutokuwa na amani dhidi ya
maendeleo ya biashara yangu. Ndio maana unapaswa kila wakati kuwa
mwangalifu na mawazo yako na vizuri kufikiri kwa kina na chanya zaidi
kabla ya kuchukua maamuzi yoyote yale.
Jiulize ni kwa nini umeshindwa kuanza biashara? Ni kwa nini
unashindwa kuonana na mtu unayejua fika ni mtu anayeweza kukusaidia
katika hatima njema ya kufikia ndoto yako? Nataka nikuambie umekosa
ujasiri bado unatanguliza hofu mbele yako, na hii ndio sababu ya wewe
kushindwa kuendelea mbele na kufanikiwa katika maisha yako. Amua kuanzia
sasa kuwa miongoni mwa watu wenye kiu na shauku ya juu ya mafanikio ili
uweze kufikia kilele cha ndoto yako uliyonayo.
Post a Comment