Na. Ahmad Mmow, Lindi.
Tabia
ya baadhi ya wanaume kushindwa kuwapa ushirikiano wake zao wanapokuwa
wajawazito imetajwa kuwa inachangia vifo kwa akina mama wajawazito na
watoto wachanga.
Hayo
yameelezwa leo na muuguzi msitahafu, Faith Nipwapwacha katika siku ya
kwanza ya warsha ya siku mbili kuhusu namna ya kupunguza vifo vya akina
mama wajawazito na watoto wachanga.
Nipwapwacha
ambae alikuwa ni miongoni mwa wawezeshaji wa warsha hiyo alikemea tabia
ya baadhi ya wanaume kuwazuia wake zao kuhudhuria kliniki na kuwapa
huduma za msingi wanapokuwa wajawazito.
Badala
yake wanakuwa wepesi wa kuchangia na kuandaa gharama za mazishi pindi
vinapotokea vifo vya akina mama na watoto wachanga. Alisema vifo vya
akina mama wajawazito na watoto wachanga vinaweza kuepukika iwapo jamii
hasa wanaume wakibadili mtazamo. Kwasababu vifo vingi vinatokana na
sababu zinazoweza kuzuilika.
Akibainisha
kuwa kuwasaidia akina mama wajawazito ni hatua muhimu katika kupunguza
vifo hivyo. Hata hivyo uzoefu unaonesha baadhi wanaume nikwazo katika
kuwafanya wake zao kihudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Badala yake wanakuwa na huruma na kuonesha upendo kwa maiti kwa kufanya gharama kubwa za mazishi.
"Utawaona
akinababa wamejazana kwenye gari kufuata maiti ya mama mjamzito,
wanachingia pesa nyingi kwa ajili ya mazishi, lakini mama huyo angekuwa
anahudhuria kliniki asingepoteza maisha," alisema Nipwapwacha.
Alibainisha
kwamba alipokuwa mtumishi wa umma kwa nafasi yake ya uuguzi alibaini
kwamba vifo vingi vya akina mama wajawazito na watoto wachanga
vinasababishwa na kukosa mahitaji ya msingi, ambayo kwa kiasi kikubwa
yanapatikana kirahisi katika maeneo wanayoishi na kwenye vituo vya
kutolea huduma ambako wangeweza kupata ushauri na baadhi ya dawa. Ikiwamo vidonge vya kuongeza damu.
Huku
akitoa wito kwa jamii kuguswa na vifo hivyo na kutambua kuwa kuwasaidia
wajawazito ni njia bora ya kuokoa uhai wao. Badala ya kuona ni jambo la
kawaida.
Alisema jamii inawajibu wa kuchangia mahitaji ya msingi kwa wajawazito wanapokaribia kujifungua.
"Akina
mama wengine wanafariki kutokana na upungufu wa damu, lakini jamii
inauwezo mkubwa wa kuondoa tatizo hilo iwapo itachangia. Lakini pia
vijiji vingine havina zanahati na wanaume wengine uwezo wao ni mdogo,
maeneo kama hayo kuna umuhimu wa kuchangia gharama za usafiri kumfikisha
zahanati badala ya kusubiri kuchangia kwa ajili ya kurudisha maiti," aliongeza kusema Nipwapwacha.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake na
watoto mkoa wa Lindi (LIWOPAC), Cosma Bulu, aliwaasa akina mama
wazitambue haki zao, wazidai na wapaze sauti pindi wanapoonewa na
kunyanyaswa na waume zao.
Akibainisha kuwa akina mama wengi wanadhulumiwa haki zao. Hata hivyo wanashindwa kulalamika na kuomba msaada.
Warsha
hiyo ya siku mbili inafanyika katika manispaa ya Lindi na
kuwashirikisha baadhi ya wananchi wa vijiji vilivyopo kata za
Nyangamara, Milola na Nangaru yameandaliwa na LIWOPAC kwa ufadhili wa
shirika la kuhudumia asasi za kiraia (FCS).
Post a Comment