WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imedhamiria kuwalinda watoto wa kike na ndiyo maana inasisitiza waachwe wasome
hadi wamalize kidato cha sita.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati
akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani
Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za
maendeleo.
Amesema nia ya Serikali ni kupata watumishi ambao ni
wataalamu wa kada tofauti kama madaktari, wanasheria, mafundi, walimu na hata
Wakuu wa Wilaya ambao ni wanawake.
Aidha Mhe. Majaliwa amewaonya wazazi ambao huwa
wanakubali kuongea pembeni na kupewa fedha na wanaume waliowapa mimba mabinti
zao na kuwaeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ilivyo, nao pia wanastahili kupewa
adhabu ya kifungo jela.
Akiwa kwenye baadhi ya vijiji, Waziri Mkuu ameelezwa
kwamba kuna shule ambazo zina walimu wa kiume watupu na akamtaka Afisa elimu
asimamie suala hilo kwa kuwahamisha baadhi ya walimu kutoka Ruangwa mjini na
kuwapeleka shule za vijijini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yupo
Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Post a Comment