MKAZI wa kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata ya
Masanze, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Augustino Mtitu, aliyechomwa
mkuki mdomoni na kutokea shingoni, amemshukuru Mungu, madaktari,
uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa kijiji hicho
kwa kuwezesha kunusuru maisha yake.
Mkuki huo ulimjeruhi na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro kufanyiwa upasuaji na kufanikiwa kuondolewa mkuki huo na kuokoa
maisha yake.
Mtitu (42) ambaye ni mkulima alisema hayo alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari hizi akiwa wodi namba moja, inayolaza wagonjwa wa
majeraha ya ajali katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro.
Mkulima huyo na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha
jamii ya wafugaji wa kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo
katika wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Tukio hilo lililotokea saa 5:00 asubuhi Desemba 25 mwaka huu.
Alisema licha ya sasa kuendelea vizuri, alipata maumivu makali kuanzia
muda wa kuchomwa mkuki huo na kulazimika kuushikilia mkononi mkuki
kuanzia muda huo hadi saa 10:00 jioni ya siku hiyo alipofikishwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na madaktari kumfanyia upasuaji
na kuutoa.
“Namshukuru Mungu, pia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen,
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Frank Jacob waliofika kuniona na kunifariji na
leo (jana) amenitembelea Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule na baadhi ya
ndugu zangu wa kijijini Dodoma Isanga,” alisema.
Hata hivyo, hakuweza kuzungumza mwa muda mrefu kutokana na sehemu ya
jeraha bado ikiletea maumivu, ingawa alisema si kama yaliyokuwa siku ya
kwanza baada ya upasuaji.
Katika wodi hiyo, wananchi waliokuwa wakienda kuwaanglia ndugu zao
waliolazwa walikuwa wakimiminika eneo la kitanda chake wakimjulia hali
na kumpa pole kwa mkasa huo wa aina yake.
Naye Stanley Andrea, ndugu wa Mtitu, ambaye yupo katika Hospitali ya
Rufaa ya mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema hali yake inaleta
matumaini ya kupona na kwamba kwa sasa anaweza kula vyakula laini.
IMEANDIKWA NA JOHN NDITI-habarileo MOROGORO
Post a Comment