0

KAIMU Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania(TCDC), Tito Haule, ametangaza kuondoa bodi za vyama kadha vya ushirika na kusimamia uendeshaji wa vyama hivyo. Bodi hizo ni za chama cha ushirika cha Ayalabe Saccos Ltd na Ayalabe Dairy, ambavyo vipo wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Maamuzi hayo yamefanyika katika juhudi za kuimarisha ushirika na kudhibiti ubadhirifu na matumizi mabaya ya mamlaka.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Haule alisema tume hiyo imefikia hatua hiyo kwa kuzingatia Sheria ya Vyama hivyo Namba 6 ya mwaka 2013 na taarifa za ukaguzi na uchunguzi zilizofanywa kufuatia migogoro isiyoisha katika vyama hivyo.

Alisema ilibainika katika uchunguzi huo kuwa kuna ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka, ulioambatana na uendeshaji mbovu kwa takribani miaka mitatu.

Aidha alisema imebainika kwamba baadhi ya tuhuma ni za kuingia mikataba isiyo na tija bila idhini ya Mrajis, kinyume na sheria ya vyama vya ushirika ya mwaka 2013, na kutoandaa hesabu za vyama kwa ajili ya ukaguzi. Pia bodi hizo zimefanya matumizi yasiyo na makisio, yaliyoidhinishwa na Mrajis kinyume na sheria ya vyama hivyo.

Katika usimamizi huo, Tume itasimamia malipo ya mikopo kutoka taasisi za fedha na serikali na pia shughuli za kiwanda cha usindikaji maziwa. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu ubadhirifu wa kiasi gani umefanyika, alisema bado haujabainika hadi hapo vyombo vya dola vitakapokamilisha uchunguzi wake.

Alisema Usalama wa Taifa, Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), bado zinaendelea na uchunguzi wake kwa lengo la kuwachukulia hatua wale wote watakaokuwa wamepatikana na hatia ya kuhusuika na ubadhirifu huo.

Haule alisema Tume itaitisha mkutano mkuu wa wanachama mara baada ya uteuzi wa Bodi za mpito kwa lengo la wanachama kuidhinisha Bodi hizo na kupata taarifa hatua zilizochukuliwa.

Alitoa mwito kwa viongozi wa vyama vya ushirika na wasimamizi nchini, kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa Tume haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kiutawala kwa wale wote watakaobainika kufanya wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Post a Comment

 
Top