Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama
Janeth Magufuli, leo wameungana na waumini wa Jimbo Katoliki la Singida kusali
Misa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatatifu wa Yesu
Mjini Singida.
Misa
hiyo Takatifu ya Krismasi imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida
Mhashamu Edward Mapunda.
Akizungumza
mara baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri
ya Krismasi waumini wote wa Jimbo la Singida na Watanzania wote kwa ujumla na
amewasihi kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu kwa kuendeleza amani na upendo
na kuacha vitendo vya kubaguana kwa misingi ya dini, kabila, itikadi na kanda
zao.
Katika
hatua nyengine Dkt. Magufuli amewahimiza Watanzania wote kuongeza juhudi katika
kuchapa kazi kama alivyofanya Bwana Yesu na pia amesema kwa kuwa maeneo mengi
ya nchi yameonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua, ni vyema wakatumia vizuri mvua
chache zinazoendelea kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka
upungufu wa chakula.
Kwa
upande wa Mkoa wa Singida ambao ni maarufu kwa kilimo cha alizeti, Mhe. Rais
Magufuli amewasisitiza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda ambayo nchi
inatoa kipaumbele kwa kuzalisha alizeti kwa wingi ili zitumike kuzalisha mafuta
mengi ya kupikia.

Post a Comment