Na
mwanishi wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na
kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani kwa kuwa hakuna
madarasa ya kutosha.
Ametoa kauli hiyo jana mchana wakati
akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lindi mara baada ya kupokea
taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa na madawati ya
kutosha kurudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote
waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza kutokana na
wanaokwenda chaguo la pili kuwa wamechelewa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema atafuatilia kubaini ni
kwa nini taasisi ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi
mazao kwenye maghala hayo.
Waziri Mkuu amesema atapitia sheria ya
kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama inaruhusu tozo hizo na kuangalia
sheria gani inawaruhusu kutoza kodi. Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali
inatoza tozo kwenye maghala ambayo yamejengwa na wananchi.
Waziri Mkuu amesema kama Serikali
inaruhusu kuwepo kwa tozo hizo kwa jambo ambalo wananchi wamelibuni wenyewe,
basi ilipaswa kudai kodi na hiyo kodi ilitakiwa kukusanywa na Mamlaka ya mapato
Tanzania (TRA) na siyo vinginevyo.
Waziri Mkuu amesema atafuatilia wakala
mbalimbali walioanzishwa kwenye wizara kwani kuna nyingine zinafanya kazi
ambazo zilistathili kufanywa na idara kwenye wizara mama.
Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea
akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.

Post a Comment