MOTO
mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba zaidi ya 50 katika kisiwa cha
Kasalazi kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani
Mwanza.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku, linadaiwa kuwa ni la nne kutokea kisiwani humo katika miaka ya karibuni.
Imeelezwa kuwa moto huo ulizuka na kuteketeza nyumba hizo huku wamiliki wake wakiwa kwenye shamra shamra za Krismasi.
Nyumba zilizoteketea kwa moto ni zile zilizojengwa kwa kutumia mabanzi
ya miti, mbao na kuezekwa kwa maturubai, nyasi na baadhi kwa bati.Chanzo
cha moto huo bado hakijafahamika.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasalazi, Andrew Mkama, amesema kuwa wakati
tukio hilo linatokea, wakazi wengi wa kisiwa hicho walikuwa kwenye
kumbi mbalimbali za starehe kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi
ya miaka 2,000 iliyopita.
Mkama alisema alilazimika kupuliza filimbi kuashiria hatari na wananchi
walijitokeza na kuanza jitihada za kuuzima moto huo licha ya kwamba
tayari ulikuwa umeshasababisha madhara makubwa kwa kuunguza mali zote
zilizokuwa ndani yake.
Hata hivyo alisema hakuna mtu aliyekufa wala kujeruhiwa kutokana na janga hilo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo umesababisha hasara kubwa kwao.
Mmoja wa mashuhuda hao, Raphael Bituro, anayemiliki duka la vinywaji,
alisema baada ya kupulizwa filimbi kuashiria hali ya hatari, baadhi ya
wateja wake walikurupuka bila kulipia vinywaji vyao na hivyo kusababisha
apate hasara.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alithibitisha kisiwa hicho kuungua kwa moto.
Kipole alisema ameagiza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini ukubwa wa
madhara hayo na kuahidi kutoa taarifa zaidi atakapopewa ripoti hiyo.
Kisiwa hicho kinakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 2,400 ambao
hujihusisha na shughuli za uvuvi na ni miongoni mwa visiwa vinane
vilivyopo kwenye Kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema
Post a Comment