RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa si vyema misikiti kuwa chanzo
cha mizozo, mivutano na migongano na badala yake iwe sehemu ya kuwaunganisha
Waislamu kwani hayo ndio mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Dkt. Shein ameyasema hayo jana mara baada ya ufunguzi wa masjid Muhammad
(S.A.W) uliopo Fujoni Mzambarauni, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini
Unguja.
Akitoa nasaha zake kwa waumini wa dini ya Kiislamu wa Fujoni na vijiji vya
karibu, Dkt. Shein ameeleza kusikitishwa kwake na tukio lililofanywa na baadhi ya waumini wa Kiislamu hivi karibuni
huko kisiwani Pemba la kuchoma moto msikiti, kuiba mashine ya kupandishia maji
sambamba na baadhi ya waumini kubaguana katika baadhi ya misikiti.
Amesema kuwa misikiti ina mchango muhimu katika kuwaunganisha wanajamii
wanaosali pamoja na huwapelekea kujuana na kushirikiana katika masuala mbali
mbali na kusisitiza umuhimu wa kuitunza misikiti ukiwemo msikiti huo mpya ambao
una sifa zote.
Dkt. Shein amesema, kuwapatia watoto
elimu ni jukumu la kila mzazi, hivyo wazazi pia wanapaswa kuwa na ushirikiano
na walimu kwa kila hali ili wapate moyo wa kuitekeleza kazi yao ambayo
inajulikana kuwa ni ngumu.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wale wote
walioshiriki katika ujenzi wa msikiti huo azidi kuwafunguliwa milango ya riziki
bna watilie baraka katika kufanya shughuli zao.
Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la
Mahonda Alhajj Balozi Seif Ali Idd, ameeleza
juhudi zilizochukuliwa katika kuhakikisha mfadhili wa ujenzi wa msikiti huo
anapatikana ikiwa ni pamoja na kutimiza ahadi yake ya kutafuta mfadhili wa
msikiti huo.
Nao wananchi wa Shehia ya Fujoni katika risala yao walieleza furaha yao kwa kujengewa msikiti huo mpya
ambapo walieleza kuwa hapo kabla msikiti uliokuwepo ulikuwa haukidhi haja
kutokana na udogo wake, uchakavu sambamba na kwenda masafa marefu kufuata
misikiti kwa ajili ya sala za Idd na Ijumaa.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, viongozi wa dini ya kiislamu, wananchi na
wageni kutoka ndani na nje ya Zanzibar walihudhuria katika ufunguzi huo wa
masjid Muhammad (S.A.W).
Post a Comment