0


Na mwandishi wetu Zanziab

Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amezipongeza Serikali za Oman na ile ya Cuba kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo sambamba na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na nchi hizo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na Mabalozi wa nchi hizo Ikulu mjini Zanzibar hapo jana, Dk. Shein amezipongeza nchi hizo kutokana na ushirikiano wanaoutoa na kuutaja kuwa chachu katika kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujileta maendeleo.
Awali akizungumza na Balozi wa Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  bwana Jorge Luis Lopez Tormo ambae kwa sasa  amemaliza muda wake wa kazi hapa nchini, Dk. Shein ameeleza kuwa mbali na madaktari kutoka katika nchi hiyo ambao wamekuwa wakija nchini kusaidia katika sekta ya afya tangu 1964, Cuba imekuza uhusiano wake kupitia sekta hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo kuanzisha chuo cha Udaktari ambacho tayari kimeshaanza kuzalisha matunda kwa kutoa Madaktari Wazalendo.
Aidha, amesema kuwa mbali ya kuimarisha  ushirikiano katika sekta ya afya kwa nchi hizo mbili ameelezea azma ya kuanzisha ushirikiano katika sekta ya utalii kutokana na Cuba kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Nae Balozi Jorge Luis Lopez Tormo alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa Cuba itaendeleza miradi yote ya maendeleo inayoishirikisha nchi yake huku akiweka wazi kuwa nchi yake itafarajika kwa kuwepo ushirikiano katika sekta ya utalii.
Amesema kuwa kwa mwaka huu pekee,  Cuba imeweza kupokea watalii wapatao milioni tatu na nusu na kukiri kuwa mfanano wa miji mikongwe ya Zanzibar na Havana unaweza kuwa chachu katika kukuza utalii kwa pande zote mbili.
Katika hatua nyengine Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo mpya wa Oman, Ahmed Bin Humoud Al Habsi, ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Oman kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo.
Dk. Shein ameeleza kuwa miongoni mwa juhudi zilizochukuliwa na Oman katika kuisaidia Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Afya kilichopo Mbweni pamoja na fedha taslim kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, msaada wa gari kwa ajili ya viongozi wa Serikali na misaada mengine ambayo nchi hiyo imeshawi kuitoa.

Post a Comment

 
Top