Baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza
kutupilia mbali maombi ya wananchi wanne wa kutaka itengue ushindi wa
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema), walalamikaji hao
wamesema watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kwa kile walichosema
kuwa Mahakama hiyo haikutenda haki katika kutoa maamuzi hayo.
Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyokuwa
inasikiliza kesi hiyo namba moja ya mwaka huu, katika Mahakama ya Mkoa
wa Mara mjini Musoma, chini ya Jaji Noel Chocha, ilitupilia mbali kesi
hiyo na kumthibitisha Bulaya kuwa ni Mbunge halali wa jimbo hilo.
Wananchi hao wanne walikuwa wamefungua kesi hiyo wakipinga ushindi wa
Bulaya dhidi ya Stephen Wasira kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa waandishi wa habari walimhoji mmoja wa
walalamikaji Janes Ezekiel, ambaye alisema kuwa watakaa na wenzake waone
namna ya kukata rufaa.
Hata hivyo baadaye mlalamikaji mwingine Ascetic Malagila alimwambia
mwandishi wa habari hii kuwa tayari wamekubaliana na wenzake pamoja na
mwanasheria wao kuwa watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga
hukumu hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa wameshindwa kwa sababu ya uonevu
na kwamba watatafuta haki yao katika Mahakama ya Rufaa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Wasira alidai kuwa tayari
walalamikaji hao pamoja na wakili wao Constantine Mutalemwa, wamekutana
na kukubaliana kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kutafuta haki.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa Jaji Chocha, alirejea baadhi ya vifungu
vya sheria pamoja na hoja mbalimbali zilizotolewa na waleta maombi
(walalamikaji) na wajibu maombi wa kwanza, wa pili na watatu.
Jaji Chocha alisema kuwa kutokana na kupitia vifungu vyote vya sheria
pamoja na ushahidi uliotolewa na waleta maombi katika Mahakama hiyo, ni
kwamba ushahidi wao haujajitosheleza katika hatua ya kutengua ubunge wa
jimbo hilo.
Alisema kuwa iwapo ataamua kufuta matokeo hayo atawasababishia wananchi
wa jimbo hilo ambalo ni miongoni mwa jimbo lenye watu masikini sana
kukosa haki yao.
Alisema kuwa madhara ya kurudia uchaguzi ni makubwa sana, sanjari na
gharama za uendeshaji wa uchaguzi mpya, ambao utaligharimu taifa na
wananchi kwa ujumla kwa sababu gharama za uchaguzi ni sehemu ya kodi ya
kila mwananchi.
Akirejea mwenendo mzima wa kesi hiyo tangu ilipofunguliwa katika
Mahakama hiyo, Jaji huyo alikiri kutokea kwa kasoro kadhaa katika
kipindi cha uchaguzi hadi kutangaza matokeo na kusema kuwa ni kawaida ya
uchaguzi wowote kuwa na kasoro ndogondogo na kuongeza kuwa hata nchi
zilizoendelea kasoro huwa hazikosekani.
Alisema kuwa katika kesi hiyo kasoro nyingi zilizojitokeza zimeonekana
mara baada ya matokeo kutangazwa, lakini katika mchakato mzima wa
upigaji kura hakuna kasoro zilizobainishwa, ambazo zingeweza kuonekana
kwenye fomu yoyote ya malalamiko anayokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi,
ambazo zingeonesha kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki. Alibainisha
kuwa si kila kasoro inayojitokeza kwenye uchaguzi inaweza kuathiri
matokeo ya uchaguzi.
Hata hivyo alisema kuwa pia msimamizi wa uchaguzi huo Lucy Msoffe
alifanya uzembe mkubwa sana wakati alipofika katika hatua ya kuandika
idadi ya wapiga kura na kwamba alipaswa kuwa makini kwa kutokuandika
takwimu kimakosa.
Akizungumza nje ya Mahakama hiyo wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja,
alisema maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hiyo waliyatarajia tangu mwanzo
wa kesi hiyo kwa sababu hakukuwa na hoja zozote za msingi za waleta
maombi.
Kuhusu gharama walizotumia katika kesi hiyo wakili Kipeja alisema kuwa
watakaa pamoja na wakili Tundu Lissu, ili waweze kurudishiwa gharama zao
zote walizotumia kuendeshea kesi hiyo.
Post a Comment