|
RAIS wa
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jaji Slivia Fernandez de
Gumendi, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi.
Katika
mazungumzo hayo ya Jaji Gumendi na Balozi Manongi, Rais wa ICC
aliishukuru Tanzania kwa hotuba yake iliyotolewa na Balozi siku ya
Jumatatu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili
Ripoti ya ICC.
Kwa
mujibu wa Gumendi, hotuba hiyo ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano
(balanced) na pia ilitoa ushauri au mapendekezo ya namna gani Mahakama
hiyo, inavyoweza kuboresha uhusiano na wanachama wake kwa mujibu wa
Mkataba wa Roma.
“Nilikusikiliza
kwa makini sana wakati ulipokuwa unatoa hotuba yako, nilinukuu kila
hoja ulizokuwa unazizungumza. Hotuba ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano
(balanced) na ningependa kuitumia fursa hii kuishukuru Tanzania kwa
hilo,” alisema.
Rais huyo
wa ICC alikiri kwamba anadhani ni wakati muafaka kwa wadau wa pande
mbili, kukaa na kuzungumza kama ambayo Tanzania na wanachama wengine
wameshauri, hasa kutokana na kile alichosema kwamba kila nchi imekuwa na
tafsri tofauti na uelewa tofauti kuhusu baadhi ya vipengele (articles),
vinavyohusu Mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai.
Kwa
upande wake, Balozi Manongi alisema ushauri na mapendekezo ambayo
yametolewa na Tanzania pamoja na nchi nyingine, hayalengi katika kutaka
kubadili Mkataba wa Roma au kuipunguzia nguvu ya kiutendaji mahakama
hiyo.
“Tungependa
sana ieleweke kwamba tunaposhauri kukaa na kuzungumza, kusitafsiriwe
kana kwamba tunataka kupunguza nguvu ya utendaji wa chombo hiki, ambacho
wote tunaamini kwamba kinastahili kuwapo. Tunachosema na kusisitiza ni
kwamba kila upande una hoja za msingi, basi tuzijadili kwa kuzungumza,”
alisisitiza Balozi Manongi.
Rais huyo
wa ICC na Balozi Manongi, walibadilishana mawazo juu na masuala
mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya ICC, ikiwa ni pamoja na
kuangalia ni maeneo gani ambayo Mahakama na wanachama wake wanaweza
kujadiliana.
Post a Comment