0

WAKATI mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) akifikishwa mahakamani kwa mashitaka ya ugaidi mkoani Dodoma, wadau wanaotetea haki za wanawake na watoto wamelaani kitendo cha wanawake wanne na watoto kukamatwa wakijihusisha na mafunzo ya ugaidi na kuiomba serikali kuchukua hatua kali kwa wahusika.
Juzi Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupitia Kikosikazi kinachopambana na uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi, kiliwakamata wanawake wanne na watoto wanne kwa tuhuma za kujihusisha na mafunzo ya ugaidi katika maeneo ya Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Happiness Bagambi alisema matukio kama hayo yanachangiwa na wazazi kutokujua wajibu wao.
“Kitendo cha kuwachukua watoto na kuwapeleka kwenye mafunzo ya kigaidi ni ukatili kama ukatili mwingine, tena huu umepitiliza… sisi tunachopaswa ni kuwalea watoto na kuwapa haki zao ikiwemo elimu ila hili lililofanyika ni kuwaharibia maisha,” alisema Bagambi.
Alisema wahusika wa hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria na waadhibiwe kama wabakaji au wahalifu wengine kwa sababu mambo hayo siyo ya kuvumilia katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Watoto (TAJOC), Raphael Kibiriti alisema chama hicho kinalaani kitendo hicho kwa kuwa wazazi na walezi kuwatoa watoto katika mikono salama na kuwapeleka katika vitendo hivyo ni ukatili uliopitiliza.
Aliiomba serikali kuchukua hatua kwa wahusika wote waliowatoa watoto kwenye mikono salama na kuwaingiza katika vitendo hivyo sambamba na kuiomba serikali kuwasaidia watoto hao kurudi shuleni kuendelea na masomo yao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema watoto hao wanne walikuwa wametoroshwa kutoka katika familia mbalimbali ikiwamo ya Shabani Abdala Maleck ambaye ni mkazi wa Kitunda.
Watoto hao ambao walikuwa wameachishwa katika shule mbalimbali nchini, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu ikiwemo karate, kumfuu na judo pamoja na kufundishwa jinsi ya kutumia silaha aina ya SMG na bastola.
Mkoani Dodoma, mtu anayehusishwa na vitendo vya ugaidi, Azan Abubakary amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini na kusomewa mashtaka yake.
Akiwa amevalia fulana ya rangi ya bluu na kijani na suruali nyeusi na viatu vya matairi (maarufu kama katambuga), alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mwajuma Lukindo.
Mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa makosa ya kufadhili ugaidi chini ya kifungu cha 13 cha sheria ya makosa ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002. Ilidaiwa kuwa Mei 15, 2016 alimtumia fedha Mohamed Ibrahim kwa njia ya M-Pesa kiasi cha Sh 265,000 katika namba +254 708104109 kwa ajili ya kufanyia ugaidi nchini.
Aidha Julai 22, 2016 Abubakary alionekana eneo la Dodoma akituma fedha kwa njia ya M-Pesa kwa Mohamed Ibrahim Sh 148,000 kwa ajili ya kufanya vitendo vya ugaidi. Hakimu Lukindo alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma katika taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema kwamba mtuhumiwa huyo aliyefikishwa mahakamani ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo cha Afya na yupo mwaka wa pili.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, mtuhumiwa alikamatwa Nzega mkoa wa Tabora baada ya kugundulika kuwa anajihusisha na mtandao wa ugaidi wa kundi la ‘Al Shabaab’ kutoka Somalia.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikamatwa kutokana na taarifa za Intelijensia ya Polisi katika masuala ya ugaidi. Katika tukio lingine, polisi wanafanya uchunguzi wa kifo cha mashaka kilichotokea Novemba 15, mwaka huu saa 12 jioni katika Hoteli ya Kitemba katikati ya mji wa Dodoma.
Katika tukio hilo, Ofisa mstaafu wa Magereza aliyefahamika kwa jina la DCP – Luvugo Chiza, mwenye miaka 62, mkazi wa Kigoma aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Kigoma, alishuka Dodoma na kulala katika hoteli hiyo kwa ajili ya kushughulikia viwanja vyake CDA.
Ofisa huyo alikutwa amefariki dunia huku akitokwa na damu puani, pia katika chumba chake yalikutwa mabaki ya vyakula, chips, nyama ya kuku, nyama ya nguruwe, chupa ya maji na kinywaji aina ya Savana.
Imeandikwa na Hellen Mlacky (Dar) na Sifa Lubasi (Dodoma).

Post a Comment

 
Top