Tangulia Spika wa Bunge la Wananchi
Hotuba ya ndugu Kiongozi wa ACT Wazalendo katika Kikao Maalumu cha Bunge cha Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta
Ndugu Spika,
Ndugu Wabunge,
Mama Magreth Sitta,
Watoto wote wa Mzee Samwel John Sitta, Ndugu, Jamaa na Marafiki,
Ndugu zangu Watanzania,
Ndugu Wabunge,
Mama Magreth Sitta,
Watoto wote wa Mzee Samwel John Sitta, Ndugu, Jamaa na Marafiki,
Ndugu zangu Watanzania,
Leo
kikao maalumu cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika
Mkutano wake wa Tano kinamuaga mtoto wa Mzee John Sitta na Hajjat Zuwena
Said Fundikira. Nami nimepewa nafasi niseme maneno machache kuhusu mzee
wetu huyu tunayemuaga.
John
Samwel Sitta anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu
aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu, shujaa wa wote
wanaoamini katika Uwajibikaji wa kitaasisi, Mwanasiasa aliyepanda na
kushuka na kisha kupanda na kubakia kileleni, taswira ya mkoa wake wa
Tabora, sio tu mdhamini wa klabu ya Simba, bali pia Mwanasimba
aliyeipeleka klabu Brazil na kuwezesha kuifunga Yanga mabao mengi zaidi
ambayo hayajapata kulipwa na wapinzani wetu hata kwa kuungakuunga,
Mwanamageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania.
Hata
katika kifo chake, Samwel John Sitta ameweka rekodi nyengine – kwa
Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya
mwaka 1975 – 2015 isipokuwa tu kwa kipindi cha 1995 – 2005. Rekodi hii
itaendelea kwa wengine wote watakaofuata baada yake.
Ni
mtu wa namna gani wewe Samwel Sitta? Spika wa Kasi na Viwango,
unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya Jeneza lako lililopambwa na
Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo kwenye nyumba
yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako
hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu (The Peoples
Speaker).
Tuliokupenda
tunajua. Ulikuwa Baba mlezi. Ulikuwa Mume mwema. Ulikuwa Babu. Ulikuwa
Kiongozi. Nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo.
Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa katika kukukumbuka
ewe Spika wa Watu.
Ulikuwa
na vyeo vingi; Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Waziri tena,
Mkurugenzi Mtendaji, Spika, Waziri tena na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu
la Katiba. Lakini, wala, tunakuita Spika Sitta tu. Kwanini? Kwa sababu
‘Legacy’ yako ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sio
kwamba umeanzisha Bunge wewe, la hasha. Lakini ulipopokea Uspika wa
Bunge letu, kama ilivyo jadi yako, uliliboresha, uliwezesha kutunga
kanuni mpya, uliimarisha Mhimili huu na kuuweka katika nafasi yake ya
Kikatiba.
Nakumbuka
siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aongee na
baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006. Mimi nikiwa nina miaka 29 tu.
Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa
kumshawishi Rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia;
“Babu, mimi sasa alasiri, ninyi ndio saa nne asubuhi. Nawawekea misingi tu na kuliweka Bunge katika nafasi yake ya kikatiba”.
Kilichofuata
ni mabadiliko makubwa ya Kanuni za Bunge, kuandikwa upya kwa Sheria ya
Bunge (National Assembly Administration Act, 2008) na kuanzishwa kwa
Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo, Constituencies Development Catalyst Fund
(CDCF).
Samwel
Sitta, bado tunasikia mwangwi wa sauti yako nene kutoka kwenye kiti cha
Spika ukiwataka Mawaziri wajibu maswali kwa ufasaha. Hukuisahau Tabora
yako. Damu ya kichifu wa Unyanyembe ya Fundikira kutoka mama yako Zuwena
ilikusambaa kwenye mishipa yako. Ukiona kuna swali linalohusu mkoa wako
wa Tabora hukusita kuwaambia Mawaziri wajibu vizuri (haswa kuhusu
barabara), au ukiamsha jeshi lako (akina Lucas Lumambo Selelii nk)
wakisema “mheshimiwa Spika, wewe leo ukipata dharura Urambo unafikaje!”.
Yote hiyo kutilia nguvu umuhimu wa maendeleo ya mkoa wako.
Wewe
ni kielelezo cha Demokrasia ya Vyama vingi bungeni. Ulitoa nafasi kwa
wabunge wote wa kambi zote ndani ya Bunge. Hatusemi hukubagua, la hasha,
uCCM wako ulikuwa pale pale. Lakini walio wengi walishinda na walio
wachache walisikika. Ndio Demokrasia hiyo.
Sitta
ulikuwa Muungwana. Nakumbuka siku ile unamwomba radhi Mzee John Momose
Cheyo katika kamati ya Uongozi (baada ya kuwa ulimtoa kwa makosa
bungeni), eti msongo wa mawazo ulikujaa kwani watu wanapitapita Jimboni.
Lakini uliwashinda. Unyenyekevu wako wa kuomba radhi unapokosea ni somo
kubwa sana kwa Viongozi wengine tuliobakia.
Wabunge
wenzangu, tunataka kumuenzi Spika wa Watu – Samwel John Sitta? Basi
hakuna kumuenzi bora zaidi kama kuimarisha uhuru na heshima ya Bunge
letu.
Tuendeleze Jahazi.
Samwel
Sitta anakwenda kwenye nyumba yake ya milele akiongozwa na imani yake
kubwa kwa Mungu na uzalendo wake usio na mawaa kwa nchi yake Tanzania.
Angalau bado ataendelea kuwa nasi kwa kutuachia mafundisho makubwa
kutokana na Maisha yake, mambo mema aliyoyafanya kwa nchi yetu, ndoto
aliyoiishi ya Tanzania imara na yenye heshima, na malezi kwa viongozi
wengi vijana aliowafunda na kuwalea kiuongozi.
Ni
dhahiri umeishi maisha yako Babu. Kama isemavyo biblia, 2 Timotheo 4:7
“Nimepigana Vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda”.
Tangulia Spika wa Watu (The Peoples’ Speaker) Samwel John Sitta.
Mola akulaze pema.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 11, 2016
Dodoma
Novemba 11, 2016
Dodoma
